
Imani hizo zimesababisha watu watano kuzikwa wakiwa hai, masoko kuungua, watu kuchunwa ngozi na kujeruhiwa kwa nondo.
Siri ya migogoro na matatizo ya vurugu mkoani
Mbeya yakiwamo ya kuungua kwa masoko imefichuka, baada ya machifu
kupitia Taasisi ya Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata) kugundua kuwa ni
ushirikina uliokithiri wa wafanyabiashara. Machifu wanasema vitendo
hivyo kwa kiasi kikubwa vinachangia kuvuruga kasi ya maendeleo ya mkoa
huo.
Kwa mujibu wa Mujata, hata viongozi nao hasa wale
wa kisiasa wanachangia kuwepo kwa hali tete mkoani humo, kwa kushindwa
kuwapa taarifa wananchi, huku wengine wakijiingiza katika ufisadi
kupitia wananchi.
Masoko kuungua mara kwa mara
Mwenyekiti wa Mujata nchini, Chifu Shayo Masoko
anasema chanzo cha masoko kuungua mkoani humo, ni kuwepo kwa imani za
kishirikina miongoni mwa wafanyabiashara wanaolezwa na waganga kuwa
wakichoma moto mali zao na za wenzao watapata utajiri zaidi.
Taarifa zilizopo tayari masoko manne mkoani humo
yameshaungua moto, japo vyanzo vyake havikuwa vikihusishwa na imani za
kishirikina. Kwa mfano, mwaka 2006 Soko Kuu la Mkoa wa Mbeya la
Mwanjelwa liliteketea kwa moto katika mazingira ya kutatanisha na
kuwafanya wafanyabiashara karibu 800 kuhamishiwa kwenye eneo la Sido
ambapo walijenga vibanda vya soko jipya, lakini likaungua tena baada ya
mwaka mmoja.
Mwaka 2009 Soko la Tunduma liliko mpakani mwa
Tanzania na Zambia liliungua na baadaye mwaka 2010 soko kongwe la
Uhindini jijini hapa liliteketea kwa moto katika mazingira ya
kutatanisha.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam
Mtunguja anasema Serikali inaamini kwamba masoko ya Mwanjelwa na
Uhindini yaliungua kutokana na hitilafu ya umeme, wakati lile la Sido
liliungua kwa moto wa mama lishe.
Kwa upande wa Mujata, Chifu Masoko anasema
kutokana na kukithiri kwa matukio hayo, viongozi wa taasisi yake
walikutana na kupokea taarifa za walinzi wa kijadi, waliotoa taarifa
kwamba siri ya kuungua kwa masoko hayo ni ushirikina uliokithiri.
Walisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara
waliahidiwa kupata mtaji mkubwa kama wangeunguza moto bidhaa zao na za
wafanyabiashara wengine.
’Katika uchunguzi wa kimila tulibaini kwamba
mpango huo ulitaka kufika kwenye masoko ya Mbalizi na Wilaya ya Momba,
jambo ambalo tulilazimika kufanya mikutano ya hadhara kukemea waziwazi
tabia hiyo ya ushirikina’’ anasema.
Mitaa na sifa za kutisha
Kauli ya Mujata inashabihiana na mtazamo wa watu zaidi ya 10 wa
jijini hapa waliohojiwa kuhusu sababu za Jiji la Mbeya kuwa tishio kwa
vituko.
Watu hao ambao majina yao yanahifadhiwa wanasema
Mykoa wa Mbeya una maeneo yanayojulikana kwa sifa mbalimbali mbaya na
vituko vya aina yake.
‘’ Karibu Mbeya, lakini ujue wazi kwamba maeneo ya
Soko Matola na Block T ni ya wajane, eneo la Mbalizi ni maarufu kwa
wizi wa mafuta ya dizeli, Uyole ni maarufu kwa kufungua pipe (mabomba)
za magari yaanguke ili waibe bidhaa. Tunduma ni maarufu kwa utajiri wa
ushirikina na Mbozi ni maarufu kwa kuua na kuchuna ngozi’’, anasema
mkazi mmoja.
Maeneo mengine anayotaja ni Mwanjelwa ambalo ni
maarufu kwa wizi wa mifukoni, Airpot mjini kwa wafadhili wa kupiga
nondo, Soweto la matapeli na watengenezaji wa noti bandia, Block Q la
wafadhili wa ujambazi wa silaha, wakati mitaa ya Isanga ni maarufu kwa
uchawi.
Watu kuzikwa hai
Haya nayo siyo matukio mageni mkoani Mbeya na kwa hakika yamekuwa yakiuchafua mkoa huo.
“Mkoa huu ulishachafuliwa kwani ilizuka hata
tabia ya kuzika watu wakiwa hai kwa tuhuma za ushirikina. Maeneo ambayo
watu walizikwa wakiwa hai ni kijiji cha Maramba wilayani Mbarali,
Isyesye nje kidogo ya Jiji la Mbeya, Mkwajuni Chunya na huko wilayani
Momba’’ anasema Chifu Masoko na kuongeza kuwa tukio kama hilo
limejitokeza tena kwenye kijiji cha Mshewe kilichopo Mbeya Vijijini.
Anasema kwa kushirikiana na Serikali, Mujata
imezunguka katika vijiji na miji mbalimbali kutoa elimu na kukemea tabia
hiyo, ikiwa ni pamoja na kusuluhisha migogoro ya kifamilia, ardhi na
hata migogoro ya kisiasa na kiuchumi.
‘’Ushirikina mwingine wa wafanyabiashara
unahusisha kuua watoto, kuwaua wazazi huku wengine wakidaiwa kufuga
misukule’’, anaeleza na kusisitiza kwamba Mujata itaendelea kukemea
vitendo hivyo.
Viongozi lawamani
Kuhusu kauli za baadhi ya viongozi kwamba wakazi
wa Mkoa wa Mbeya wana tabia ya ubishi na kutaka wajitawale, Chifu
Masoko anaipinga na kusema tatizo lililopo ni wananchi kutoshirikishwa
katika uamuzi wa mambo yanayowahusu.
‘’ Kwa mfano, wakulima na wafanyabiashara wa
ndizi Rungwe waligoma kwa sababu baada ya madiwani kupokea taarifa ya
kutaka kupandisha ushuru kwa asilimia 100 hawakurudi kwa wananchi
kuwaeleza ili kupata maoni’’ anasema na kuongeza:
‘’Pia wakala wa kukusanya ushuru alipatikana kwa utata, kwani
wananchi walimhusisha na kiongozi mmoja aliyemleta wakala huyo kwa njia
za utata kutoka mkoani kwake.’’
Aidha, Chifu Masoko anadokeza pia kwamba mfumo wa
vyama vingi umechangia kuharibu maadili ya vijana, huku baadhi ya
viongozi wa kisiasa nao wakiwashawishi wananchi kuwapinga viongozi
waliochaguliwa kwa njia halali.
No comments:
Post a Comment