
Ni wazi kwamba hali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo si shwari. Kumekuwa na malumbano ya muda mrefu tena kwenye mitandao ya kijamii ambapo makada na viongozi wa chama hicho wamekuwa wakitupiana lawama.
Malumbano hayo hayakuanza leo wala jana,
yamekuwapo kwa muda mrefu. Kwanza mitandao maarufu kama vile Jamii
Forums, ilikuwa ikiinufaisha Chadema kwa kuwa mashabiki wake waliutumia
kukishambulia chama tawala, CCM kwa upande mmoja na kutiana moyo kwa
upande mwingine.
Hali kwa sasa katika mtandao huo na mingineyo
imebadilika kuwa sehemu ya kushambuliana wao kwa wao. Watu wamekuwa
wakijiita majina bandia na kushambuliana watakavyo. Hata viongozi wa
chama hicho wamekuwa wakiutumia mtandao huo kushambuliana.
Ndipo sasa linapokuja suala la Zitto Kabwe ambaye
ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kumwandikia Katibu Mkuu wake, Dk
Willibrod Slaa akitaka maelezo ya tuhuma zinazorushwa kwenye mitandao
zikimtuhumu kwa ufisadi na mkakati wa kuhujumu chama.
Haya yote yanatokea kwa sababu ya mvutano wa
madaraka uliomo katika chama hicho. Itakumbukwa kuwa mwaka 2009, Zitto
alionyesha nia ya kukitaka kiti cha uenyekiti wa chama hicho, hata hivyo
wazee wa chama hicho walimsihi ajitoe ili Mbowe aendelee na ngwe yake
ya pili.
Hata hivyo, Zitto hakuishia hapo bado amekuwa na
harakati nyingi ziwe halali au haramu, jambo linaloonkana kuwa tishio
katika uongozi wa sasa. Kuna mawili, ama uongozi wa chama unajaribu
kummaliza kupitia mitandao ya intaneti kwa kumtupia kashfa hizi na zile
au anavuna alichokipanda, yaani kutaka umaarufu kupatia chama chake.
Ni wazi kwamba Zitto tofauti na viongozi wenzake
amekuwa akitafuta umaarufu kuliko chama. Wenzake wakienda kulia, yeye
yuko kushoto, wakienda na Movement for Change (M4C), yeye yuko na kamati
hii, mara yuko safari ya hii na ile, ilimradi tu na yeye amefanya kitu
tofauti na wenzake.
Hali hii inamfanya kuonekana msaliti na pengine ndiyo sababu kashfa kama hizo zinamwandama.
Lakini kitu kimoja ambacho naona viongozi wa
Chadema hasa Mwenyekiti, Mbowe na Katibu Mkuu Dk Slaa, wanakosea ni
kutokuwa wazi kuhusu masuala yanayomwandama Zitto. Je, vitimbi hivi
anavyofanyiwa vina baraka za chama au havina?
Kama havina baraka za chama kwa nini chama
kisijiepusha navyo kwa kuvikana? Kama kweli Zitto ni msaliti kwa nini
asichukuliwe hatua za kinidhamu kama walivyowahi kushughulikiwa kina
David Kafulila.
Inawezekana kweli Zitto ni msaliti, lakini kwa
ukimya huu anapata nafasi ya kutafuta huruma kutoka kwa wanachama na
wapenzi wa chama. Ukimya huu wa Dk Slaa na Mbowe unamaanisha nini?
No comments:
Post a Comment