
KOCHA Sven-Goran Eriksson amedai kwamba alishasaini mkataba wa kuinoa Manchester United kurithi mikoba ya Sir Alex Ferguson mwaka 2002.
Kocha huyo alidai hayo kupitia kitabu chake kwamba
mabosi wa Manchester United walimfuata wakati huo akiwa anaionoa
England na Ferguson alitanganza kwamba anajiandaa kustaafu.
Kwenye kitabu hicho, Eriksson aliandika: “Nilijua
ulikuwa mtego. Nilikuwa na mkataba na England hadi fainali za Kombe la
Dunia 2006 na ningeandamwa sana kama ningevunja mkataba.
“Lakini, ilikuwa bahati kupata nafasi ya kuinoa Manchester United. Nilisaini mkataba, hivyo nilikuwa kocha mpya wa timu hiyo.”
Lakini, mwishowe Ferguson aliamua kubaki kwenye klabu hiyo kwa miaka mingine 11 kabla ya kustaafu mwishoni mwa msimu uliopita.
Kwenye kitabu hicho, Eriksson alidai pia kuwahi
kulumbana na Ferguson juu ya straika Wayne Rooney kujumuishwa kwenye
kikosi cha England kilichocheza fainali hizo za Ujerumani.
“Leif (Sward) daktari wa England na mimi
tulikutana na Ferguson na daktari wa Manchester United kwenye uwanja wao
wa mazoezi. ‘Hawezi kucheza Kombe la Dunia’, alisema Ferguson. Daktari
alileta vipimo vya X-rays na kuonyesha mfupa wa Rooney uliokuwa
umevunjika, haukuwa umepona kwa wakati.
“Wakati daktari huyo alipomaliza kueleza, Leif
alimtazama usoni na kisha akamwambia ‘Kwanini umeketi hapa na
kunidanganya?’ Leif alikuwa mmoja ya wataalamu Ulaya kuhusu majeruhi
kama aliyapata Rooney. Natamani ningemrekodi kwenye video sura ya
Ferguson ilivyokuwa wakati Leif alipokuwa akielezea kuvunjika kwa Wayne
na muda wa kucheza Kombe la Dunia.
“Leif alipomaliza kueleza, nilimgeukia Ferguson, nikamwambia ‘Samahani Alex, nitamchukua Rooney’.”
Rooney alikwenda kwenye fainali hizo, lakini
hakufunga bao lolote na kuishia kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumtendea
madhambi Ricardo Carvalho.
No comments:
Post a Comment