
.Hali ndani ya Chadema inazidi kuwa si shwari kutokana na migogoro inayozidi kupiga kambi. Safari hii ikiwa katika Kanda ya Ziwa Mashariki ambako uongozi mzima wa Mkoa wa Mara, umetimuliwa.
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, pia amefukuzwa katika kikao baada ya wajumbe kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Hatua hizo zimekuja siku kadhaa baada ya
Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kutimuliwa
katika kikao cha Baraza la Kanda ya Kaskazini, kwa madai ya kukisaliti
chama hicho.
Katika tukio la Kanda ya Ziwa Mashariki,
Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Mara, Bathlomeo Machage, amevuliwa
uongozi na nafasi yake kushikwa na Charles Leyela.
Machage anatuhumiwa kushindwa kuendesha vikao na kuzorotesha maendeleo ya chama kwa jumla.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumain Makene, alisema jana kuwa mwenyekiti huyo amesimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali.
Hata hivyo, tuhuma hizo zilipingwa vikali na
Machage ambaye alisema hatua hiyo dhidi yake ni batili kwa madai kuwa
katiba haivipi mamlaka vikao vya kanda kutimua viongozi.
Alisema yeye bado ni kiongozi halali wa Chadema mkoani Mara.
Alisema uamuzi huo uliofikiwa katika kikao cha viongozi wa Kanda ya Ziwa Mashariki, ulipaswa kufanywa na Baraza Kuu la chama.
Alisema Chadema ni chama cha watu kinachojiendesha
kwa misingi ya katiba na kwamba kwa kuzingatia hilo, uamuzi wa
kumwondoa katika uongozi unapaswa kufanywa na Baraza Kuu.Alisema mfumo
wa uongozi wa kanda ulianza hivi karibuni na kwamba kamwe kikao cha
kanda hakiwezi kumfukuza kiongozi wa ngazi ya juu kama yeye.
“Chama kina katiba na kwa mujibu wa katiba hiyo
kiongozi wa chama mkoa ni mtu anayechaguliwa na Baraza Kuu, sasa
naondolewaje na kikao cha kanda wakati kikao cha baraza hakijakaa,
sijaitwa kujieleza wala kusomewa tuhuma zangu,” alieleza Machage.
Alisema tuhuma kwamba ameshindwa kuitisha vikao, hazina msingi kwa sababu jukumu hilo ni la katibu.
Kwa upande wake, Shibuda alisema uamuzi wa kumtoa nje, ulikuja
baada ya mjumbe mmoja kutoa hoja ya kumtaka atolewe kwa madai kuwa
amekuwa wakihudhuria vikao vya CCM.
Alisema uamuzi huo ulifanyika katika kikao hicho
kilichoketi mkoani Shinyanga chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe.
Mbunge huyo alisema yeye binafsi amesikitishwa mno na hatua hiyo kwa madai kuwa hajawahi kukisaliti chama.
“Mimi siyo msaliti kwa nilichokifanya ni kutetea
haki na masilahi ya wapiga kura wangu, wakulima na wafugaji. Pale Meatu
nilipanda katika jukwaa la CCM kumweleza katibu mkuu wa chama hicho
matatizo ya wapigakura wangu, maana yeye ndiye mwenye serikali iliyoko
madarakani hivi sasa,” alisema Shibuda.
Mjumbe aliyetoa hoja dhidi ya mbunge huyo, alikuwa Ahmed Nkunda, kutoka Mwibara.
Kitendo hicho kilisababisha mvutano mkali
uliomlazimisha Mbowe kuwatuliza wajumbe na kuamua kuendesha upigaji kura
za ndiyo na hapana ili kuona wangapi waliokuwa wakiunga mkono hoja na
wale waliokuwa hawaafiki.
Baada ya kuhesabiwa kwa kura za vidole, wajumbe 90
waliunga mkono hoja na wengi 30 waliipinga. Kwa matokeo hayo Shibuda
aliamriwa kutoka ndani ya ukumbi wa kikao.
Mwenyekiti wa Chadema katika Kanda ya Ziwa
Mashariki, Silvester Nhoja, alisema Shibuda alitolewa kwa matakwa ya
wajumbe baada ya mvutano.
“Shibuda alilalamikiwa na wajumbe ambao walimtaka
atoke nje , Mbowe alilazimika kuwatuliza wajumbe na kuwataka wampe
nafasi Shibuda ajieleze lakini wajumbe waligoma na baadaye zikapigwa
kura, zlizoamua Shibuda kutolewa nje,” alisema.
Mvurugano katika chama hicho kinachoongozwa kwa upinzani dhidi ya chama tawala, umekuwa mkali katika siku za hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment