

KABLA haujakata roho, kuna vitu 50 vya michezo ambavyo unapaswa kuvifanya. Aprili 2004, Gazeti la Observer la Uingereza liliandika kuwa tukio la kwanza kati ya matukio hayo ni kutazama pambano la SuperClasico. Unalifahamu pambano hili?
Achana na uchafu wa Barcelona na Real Madrid
unaoitwa El Clasico, baba wa Clasico zote duniani ni SuperClasico wakati
Boca Juniors na River Plates zinapocheza Uwanja wa La Bambonera jijini
Buenos Aries, Argentina.
Ni pambano la machozi, jasho na damu. Ni uwanja wa
vita. Ndiyo maana, katika miaka yake yote 26 akiwa katika benchi la
Manchester United, Sir Alex Ferguson alikuwa na ndoto moja tu kubwa,
kutazama pambano la Superclassico jijini Buenos Aires.
Si pambano la Superclassico tu, Sir Alex
anaendelea kutimiza ndoto zake nyingi wakati huu akila pensheni yake.
Anataka kwenda kutazama mbio za farasi Melbourne, Australia. Anataka
kutazama tenisi Marekani katika Michuano ya US Open.
Kwa nini asifanye hivyo? Pesa inaruhusu. Anaweza
asiguse mishahara yake yote aliyokusanya Manchester United kwa miaka 26
iliyopita, lakini bado akajikuta mtu tajiri zaidi miongoni mwa wazee wa
Kiingereza tena kwa utajiri anaouvuna baada ya kustaafu kufundisha soka.
Hata baada ya miaka 26 ya kuvuna mshahara wake
Manchester United, nimegundua ndiyo kwanza pesa inazidi kutiririka kwa
Sir Alex Ferguson. Pesa inakwenda katika mkondo wa pesa.
Licha ya kustaafu kwake, kila anapoamka Sir Alex
anaingiza pesa zaidi. Kila anachogusa anaingiza pesa zaidi. Kwa sasa,
kila sehemu ambayo Sir Alex anaitwa kama mzungumzaji wa mada mbalimbali
zinazohusu soka au maisha yake ya soka, anapokea kiasi cha Dola 100,000.
Ina maana akizungumza katika sehemu tano tu anaingiza Dola 500,000,
ambazo zinatosha kuipa udhamini ligi fulani ya ukanda wa SADC (Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika).
Ni watu mashuhuri wachache wanaoweza kupokea kiasi
hicho kwa kuzungumza tu. Barrack Obama anaweza kupokea baadaye
akistaafu, lakini kwa sasa inasemekana Bill Clinton na mkewe, Hilary
Clinton wanapokea kiasi hicho.
Manchester United wamemchagua kama balozi wao
katika shughuli zao mbalimbali duniani. Unajua wanamlipa kiasi gani?
Pauni 2 milioni kwa mwaka. Unadhani anafanya kazi hiyo kwa siku 364?
Hapana. Anafanya kazi hizo kwa siku 20 kati ya siku 364.
Kwa wakati huu anajiandaa kutoa kitabu cha maisha
yake. Hapana shaka moja kwa moja kitakwenda kuwa kitabu kinachoongoza
kwa mauzo Uingereza.
Atazungumza jinsi alivyompiga kiatu David Beckham,
atazungumza alivyomsajili Cristiano Ronaldo, atazungumza jinsi
alivyokwenda kumtoa selo Roy Keane siku mbili kabla ya pambano la Ligi
ya Mabingwa Ulaya.
Unajua nini? Kabla ya kuuza aliamua kufanya
promosheni ya kitabu chake kwa kuzunguka kumbi mbalimbali kuongea maneno
machache kabla ya kuonyesha kitabu chake kitakavyokuwa.
Ndani ya saa chache tangu ratiba itangazwe, tayari tiketi zote
zilikuwa zimeisha katika miji mbalimbali ya Uingereza. Kuanzia Salford,
Glasgow, London, Aberdeen, Dublin, Preston na kwingineko tiketi zilikuwa
zimekwisha.
Watu wanataka kuona sura yake. Wanataka kusikia
sauti yake kwa karibu. Lakini kwa kufanya hivi, kila tiketi moja ilikuwa
inauzwa Pauni 40. Anatengeneza pesa!
Wakati David Moyes akiteseka na vipigo vitatu vya
Ligi Kuu katika mechi saba tu, Sir Alex Kila anachozungumza kwa sasa ni
pesa. Kila anachoandika ni pesa na kila anachogusa ni pesa.
Mtu yeyote atakayemgusa Sir Alex kwa ajili ya
kuchambua mechi za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil nadhani
atalazimika kumlipa zaidi ya Pauni 1 milioni. Kwa mara ya kwanza
anapatikana akiwa hana kazi, na wala hajiandai kwa maandalizi ya mechi
za msimu mpya.
Bao la mwisho ambalo Sir Alex atapiga ni kuanza
kuuza mali zake za kumbukumbu. Unajua atauza kiasi gani koti lake
alilochukua nalo ubingwa wa Ulaya mwaka 1999 wakati Ted Sheringham na
Ole Gunnar Solskajaer wakifunga mabao ya dakika za mwisho Nou Camp? Bei
yake itaanzia Pauni 500,000.
Unajua atauza kiasi gani viatu alivyovaa wakati
Manchester United ikiichapa Arsenal 8-2 katika Uwanja wa Old Trafford?
Unajua atauza kiasi gani kitabu chake cha kuandika takwimu za mechi
katika pambano lake la kwanza katika maisha yake ya soka Manchester
United dhidi ya Oxford?
Hivi ndivyo Sir Alex anavyotiririsha pesa. Wakati fulani unakaa chini na kuwaza jinsi ambavyo maisha hayatendi haki sana.
Wakati babu fulani mstaafu kijijini kwetu
Namasakata Tunduru akisumbuka na jembe, Sir Alex anacheza gofu New York
na pesa bado inaingia.

By EDO KUMWEMBE

By EDO KUMWEMBE
No comments:
Post a Comment