
Licha ya Serikali kupitia mamlaka husika mara kadhaa kuchukua hatua ya kukemea na kukataza matumizi ya vipodozi vyenye kemikali, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda matumizi ya bidhaa hizo yanaonekana kushika kasi katika maeneo mengi nchini.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Profesa
Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Georgia, Marekani, Kelly Lewis wa kitengo cha
Sosholojia inaonyesha kuwa asilimia 30 ya wanawake nchini Tanzania
ambayo ni sawa na wanawake milioni sita, wanatumia mkorogo wenye
mchanganyiko wa vipodozi vyenye kemikali hatari kwa afya ya binadamu.
Uchunguzi uliofanywa umegundua
kuwapo kwa njia mpya za kutengeneza mkorogo (mchanganyiko unaotumika
kubadili rangi ya ngozi na kuwa nyeupe), ambao huuzwa kwa bei nafuu huku
makundi ya wanawake wakionekana kumiminika katika soko la Tandika
kujipatia bidhaa hiyo.
Mikorogo hiyo ya kila aina ambayo hutengenezwa
kulingana na matakwa ya muuza vipodozi hujazwa kwenye ndoo zenye ujazo
wa lita tano mpaka lita 10 na kupimwa kwa kutumia kijiko cha chakula na
kuuzwa kwa bei ya Sh1,000.
Ingawa kila mmoja hutengeneza kutokana na matakwa
yake lakini wauzaji wengi wa mkorogo wametaja kuchanganya aina kadhaa za
losheni, ambazo mara kadhaa zimetajwa kuwa na kemikali ambazo si nzuri
kwa mwili wa binadamu.
Miongoni mwa losheni zinazopatikana katika
mchanganyiko huo ni pamoja na Carolite, Princess claire, Bioclaire,
Miki, Super Rico, Top lemon, Tenteclaire, Extraclaire, Caronite,
Biocarrot na nyinginezo. Kwa mujibu wa wataalamu idadi kubwa ya vipodozi
hivi vimepigwa marufuku kutokana na madhara yake kwa afya ya mtumiaji.
Kipimo kinachotumika ndiyo kimeupa jina aina hii
mpya ya mkorogo na kujulikana zaidi sokoni hapo kama ‘kijiko’ huku
maeneo mengine ya jiji ukifahamika kwa majina mbalimbali kama vile
‘king’amuzi’ na ‘king’asti’.
Mwandishi wa habari hii alishuhudia biashara hii
ya kijiko ikifanyika kwa kasi sokoni hapo, huku baadhi ya wauzaji
wakiendelea kuwajibika katika utengenezaji ili kuhakikisha watu
wanaendelea kujipatia bidhaa hiyo.
Juma Seleman ambaye ni mmoja wa wauzaji na
watengenezaji wa mkorogo huo aliweka wazi kuwa aina mbalimbali za
losheni zaidi ya 20 hutumika katika kupata mchanganyiko huo, ambao kila
mtengenezaji huwa na rangi yake kulingana na vitu anavyotumia.
“Kila mmoja ana losheni zake anazoweka ingawa mimi
huwa nachanganya kali na zile zilizopoa ili isimchubue sana mtu, lakini
wapo ambao huweka losheni kali tupu hizo huweza kuwa na madhara na
kuharibu ngozi,” alisema Seleman.
Seleman aliweka wazi kuwa wauzaji wengi wa
vipodozi wamefikia hatua ya kutengeneza mikorogo hiyo ili kuwawezesha
watu wa hali ya chini kumudu gharama na ndiyo maana huuzwa kwa bei
nafuu.
“Hii inasaidia kumrahisishia mteja badala ya
kununua losheni, sabuni na maji yake ambayo gharama yake inaweza kufika
Sh10,000 anaweza kupata kitu kizuri kwa bei ya chini ya hapo na ikawa na
matokeo mazuri katika ngozi,” alisema Seleman huku akipaka mchanganyiko
huo kuonyesha mfano.
Aidha alibainisha kuwa kwa ndoo moja ya lita 10 anaweza kuuza na
kupata pesa isiyopungua Sh laki mbili, kulingana na kasi ya mauzo na
ndoo huisha kati ya siku moja mpaka tatu.
Mmoja wa wanunuzi wa mkorogo huo aliyejitambulisha
anaitwa Mama Hamis, alisifia ubora wake na kudai kuwa umekuwa na
matokeo mazuri katika ngozi yake na kuwa mng’ao wenye mvuto.
“Nunua tu dada inakufanya unakuwa mzuri ngozi
inakuwa laini na wala hupati madhara yoyote, kwani ingekuwa na madhara
basi ningeshaona lakini tangu nimeanza kutumia sijadhurika chochote,”
alieleza Mama Hamis.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kupitia msemaji
wake, Gaudensia Simwanza, ilikiri kuwapo kwa changamoto ya baadhi ya
wafanyabiashara kutengeneza mikorogo hiyo kwa kificho, licha ya mara kwa
mara kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola.
Simwanza alibainisha kuwa asilimia kubwa ya
vipodozi vinavyotumika kutengeneza ‘kijiko’vimepigwa marufuku kutokana
na kuwa na viambato vyenye sumu, ambayo kwa kiasi kikubwa ina madhara
katika ngozi na mfumo mzima wa mwili wa binadamu.
“Tumekuwa tukitoa elimu mara kwa mara kwa wananchi
kuhusiana na madhara ya matumizi ya vipodozi hivi, na wanapaswa kujua
anayewakorogea na kuwachanganyia kemikali hana nia njema na afya zao,
waepuke na kutoa taarifa ili wachukuliwe hatua,” alisema Simwanza
Kwa mujibu wa TFDA vipodozi vyenye sumu ni pamoja
na top lemon, krimu ya princess na losheni zake, Extra clair, krimu ya
viva super lemon, clere lemon, Mekako na nyinginezo ambazo huwa na
kiambato cha Hydroguinone ambacho husababisha muwasho wa ngozi, mzio
sambamba na kusababisha mabaka mwilini.
Vingine ambavyo vimetajwa kuwa na sumu kali ya
Hydroquinone ni Carolight, G&G teint uniforme, G&G Dynamiclair,
Bioclare, Maxi white na sabuni za Miki, Jaribu, Rico, Tura, Mekako,
Movate na nyinginezo ambazo tayari zilishapigwa marufuku kutokana na
kusababisha madhara kadhaa ikiwemo kansa ya ngozi.
Vipodozi vingine ambavyo vinatajwa kuwa hatari kwa
afya ya binadamu ni pamoja na vile vilivyotengenezwa kwa kutumia madini
ya Zebaki, ambayo husababisha madhara ya ngozi, ubongo, figo na viungo
mbalimbali vya mwili.
No comments:
Post a Comment