
Kwa mara ya kwanza Rais Jakaya Kikwete amemtolea uvivu Rais wa Rwanda, Paul Kagame kutokana na kitendo chake cha kumtolea lugha za matusi baada ya kumshauri kukaa meza moja na vikundi vya waasi wa nchi yake (FDLR), huku akimtaka kuacha kukuza mgogoro usiokuwepo.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda
takribani miezi miwili iliyopita wakati akizungumza katika kikao cha
Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mapema mwaka huu, mjini
Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukijadili suala la amani ya Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa
Uganda na Joseph Kabila (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na
waasi wanaopingana na Serikali zao. Akizungumza katika hotuba yake ya
kila mwezi Rais Kikwete alisema: “Ushauri ule niliutoa kwa nia njema
kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia
ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike,”
“Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali
ya Congo , Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Museveni wa
Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais Kagame hakusema chochote pale
mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno
tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.”
Alisisitiza, “Kwa upande wangu sijasema lolote
kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka
kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi
yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha, sijafanya hivyo
kwa sababu sioni faida yake.”
Rais Kagame alitoa lugha zisizostahili dhidi ya
Rais Kikwete katika sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi ya maofisa 45
wa jeshi lake Julai mwaka huu, ambapo alisema ushauri wa kufanya
mazungumzo na waasi wa FDLR ni ujinga na haupo katika historia ya
Wanyarwanda.
“Nilinyamaza kimya kwa sababu sikupenda kusikiliza
ushauri kuhusu FDLR, kwa sababu nafikiri ni upuuzi ulioambatana na
ujinga. Hatuwezi kuacha maisha yetu kama Wanyarwanda tunavyoishi sasa.
Ushauri wa Kikwete ni sawa na kucheza na makaburi ya watu wengi ambao ni
ndugu zetu,” alisema Kagame.
Katika hotuba ya jana Rais Kikwete alisema
uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika wakati mgumu na
mtikisiko, baada ya yeye kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza
na mahasimu wao na kwamba hilo linadhihirika katika kauli zinazotolewa
na viongozi wa Rwanda.
“Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na
ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa
Tanzania ,tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na
Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani” alisema Rais Kikwete.
Alisema nchi hizo ni jirani na kila moja inamuhitaji mwenzake, hivyo lazima ziwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.
“Nasisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza
tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au
nchi yoyote jirani au yoyote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo,
kwani ni mambo ambayo hayana tija wala masilahi kwetu” alisema.
Alisema nchi hizo mbili zimekuwa zikijihusisha na
mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema, kusisitiza kwamba hiyo ni moja
ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
“Nawahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna
kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu,”
alisema na kuongeza;
“Kwangu sioni kama kuna mgogoro wa aina yoyote.
Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo ‘Two wrongs do not
make a right’ (makosa mawili hayawezi kutengeneza usahihi).
Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa
na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika
Umoja wa Afrika na hata kimataifa.”
Alifafanua kuwa alitoa ushauri huo kwa kuzingatia mila na desturi za miaka mingi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao
mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za
kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea,” alisema
Rais Kikwete.
Alisema wakati wote matatizo yanazozikabili nchi
za Afrika viongozi wote huyachukulia kama mambo yanayowahusu na kupeana
ushauri, jambo ambalo alisisitiza kuwa ni wajibu kwa viongozi.
“Iweje leo mtu kutoa ushauri ule ionekane jambo
baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa, siyo sawa hata
kidogo, Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au
kuukataa” alisema Rais Kikwete na kuongeza;
“Muungwana hujibu, “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna
haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema
yasiyokuwepo na ya uongo.”
Rais Kikwete alisema Serikali ya Tanzania haina
ugomvi wala nia mbaya na Rwanda na inapenda kuendelea na uhusiano mzuri
na nchi hiyo.
“Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo
sisi hatulijui. Sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa
kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja
kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi” alisema.
Ushauri wa Rais Kikwete kwa Rwanda pia uliungwa
mkono na Rais wa Marekani, Barack Obama wakati wa ziara yake nchini
Tanzania, alipoitaka nchi hiyo kumaliza mgogoro wake na waasi kwa njia
ya mazungumzo.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alizungumzia
jinsi nchi ilivyonufaika na ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama,
Rais mstaafu wa nchi hiyo, George W. Bush, Waziri Mkuu wa Thailand,
Yingluck Shinawatra.
No comments:
Post a Comment