
STRAIKA mpya wa Yanga, Shaaban Kondo amekaribishwa Jangwani kwa adhabu baada ya kukatwa mshahara wake kwa kosa la kucheza mechi za mchangani maarufu kama ‘chai maharage’.
Kocha Msaidizi wa Yanga Fred Felix Minziro
ameithibitishia Mwanaspoti kuwa wamemkata mchezaji huyo Sh 200,000 kwa
kosa hilo huku akimpa onyo jingine kali.
Inadaiwa kuwa mshambuliaji huyo alishindwa
kujizuia kufanya tukio hilo jioni ya Jumatatu iliyopita licha ya asubuhi
kocha wake kutoa onyo mazoezi kwa wachezaji wake kuacha tabia hiyo ili
yasije yakawakuta mabaya.
Habari zinadai zaidi kuwa Minziro alishtukia dili
la baadhi ya wachezaji wake kutakiwa kucheza ndondo sehemu siku hiyo na
alifanya makusudi kuwaita wachezaji wake wote baada ya mazoezi na
kuwausia kutofanya jambo hilo kwani ni hatari kwa afya zao endapo
wataumia na pia wanaweza kukatwa mishahara yao.
Inadaiwa kuwa Kondo na beki mmoja wa klabu hiyo
ndiyo walikuwa wakihusishwa kucheza ndondo siku hiyo lakini cha
kushangaza maneno ya kocha wake hayakumuingia vizuri Kondo na kwenda
kucheza ndondo jioni huku mwenzake akikataa kufanya hivyo kwa kuogopa
adhabu.
“Inashangaza, asubuhi nimetoka kulizungumzia jambo
hilo na kila mchezaji alisikia lakini cha kushangaza jioni mchezaji
anakwenda kucheza ndondo. Ni jambo baya sana kwani unaweza ukaumia huko,
sasa sijui unafanyaje maana unaweza ukakaa nje muda mrefu ikawa ni
hasara kwako na hata kwa klabu yako pia,” alisema Minziro.
Aliongeza: “Kweli tumemkata Sh 200,000 kama adhabu
ya kosa hilo na tumempa onyo endapo akirudia atapata adhabu nyingine
kubwa zaidi ili kukomesha vitendo kama hivi.
“Tena hii adhabu itaendelea kwa mchezaji yoyote
atakeyeonekana amekwenda kucheza mchangani (ndondo). Hii ni klabu kubwa
lazima wachezaji wake pia waishi kiprofesheno,”alisema Minziro.
Hata hivyo Kondo alipoulizwa kuhusiana na jambo hilo aligoma katakata kuelezea na kudai kuwa tuachane na hilo suala.
Yanga inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Bora
Kijitonyama na jana Ijumaa walitarajia kurudi kwenye Uwanja wa Shule ya
Loyola kujiandaa na Ligi Kuu Bara msimu ujao ambayo itaanza Agosti 24.
Yanga inanolewa na kocha msaidizi Minziro baada ya
kocha mkuu Ernest Brandts kuwa katika kozi ya ukocha nchini Ujerumani
na alitarajiwa kurejea nchini jana Ijumaa au leo Jumamosi.
No comments:
Post a Comment