
Tumelazimika tena leo kuitahadharisha Serikali na mamlaka mbalimbali zinazosimamia usafiri wa pikipiki, maarufu kama bodaboda kwamba usafiri huo sasa umekuwa janga la kitaifa. Tulitoa tahadhari hiyo mapema mwaka huu, ingawa wakati huo matatizo lukuki na ya kutisha yanayosababishwa na madereva wa vyombo hivyo vya usafiri hivi sasa yalikuwa hayajawa makubwa.
Tulitahadharisha wakati huo kwamba usafiri huo wa
bodaboda ulikuwa ukielekea pabaya kwa maana ya kuhatarisha usalama wa
abiria, wananchi wanaotembea kwa miguu na madereva wa vyombo vingine vya
usafiri barabarani. Tulisema kwamba usafiri wa bodaboda ni jambo la
kudumu kutokana na ukweli kwamba tayari umewapatia ajira maelfu kwa
maelfu ya vijana ambao wengi wao walikuwa vijiweni wakijihusisha na
vitendo vya uhalifu kama ukabaji na uvutaji bangi, hivyo hatua zozote za
kuupiga marufuku zingewasukuma vijana hao warudi mitaani na kusababisha
sintofahamu.
Sisi tuliishauri Serikali iimarishe Sumatra kwa
kuhakikisha inaweka viongozi wachapakazi, wenye uwezo, dira na mwelekeo
ili kuudhibiti usafiri huo ambao tayari ulikuwa umekielemea Kikosi cha
Usalama Barabarani. Tulishauri uwekwe utaratibu wa kuwafundisha madereva
wa vyombo hivyo sheria za barabarani ili kupunguza idadi ya vifo
vilivyokuwa vikitokea kila kukicha kutokana na ajali za barabarani.
Inasikitisha kuona kwamba sasa tatizo hilo
limepanuka maradufu na Serikali na taasisi zake husika havionyeshi
dhamira ya kupata suluhisho la hali hiyo. Sumatra ambayo ndio yenye
dhima ya kudhibiti vyombo vya usafiri imekuwa dhaifu mno kiasi cha
kushindwa angalao kuhakikisha kwamba usafiri wa bodaboda unakuwa ni
salama na madereva wa vyombo hivyo wanafahamu na kuheshimu sheria za
barabarani.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, katika
Jiji la Dar es Salaam pekee, wastani wa madereva watatu wa bodaboda
hufariki kwa ajali kila siku. Madaktari na wauguzi katika Kitengo cha
Mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamesema wameelemewa na kazi
ya kuwahudumia majeruhi wa ajali za bodaboda kutokana na idadi yao
kuongezeka siku hadi siku.
Imethibitika kwamba sio tu usafiri huo sasa
umekuwa janga la kitaifa, bali pia kwamba ajali nyingi zinazosababisha
vifo na ulemavu wa viungo zinasababishwa na madereva wa bodaboda.
Usafiri huo umekosa udhibiti na kusababisha madereva wake kufanya
watakalo. Madereva wengi wanakwenda mwendo wa kasi ya ajabu na ni chanzo
cha vurugu kila mwenzao anapopata au hata anaposababisha ajali.
Tunaambiwa vijana hao wameunda “jeshi”, hivyo wanajichukulia sheria
mkononi kwa kupiga watu kwa kutumia mapanga, visu na nondo. Wengi
wamethibitika kupata ajali wakiwa wametumia dawa za kulevya au wakiwa
wametumia pombe kali.
Waendesha bodaboda wengi ni hatari hivi sasa.
Wamejiingiza katika uhalifu wa mauaji, wizi na uporaji. Matukio makubwa
ya uhalifu kama ya kumwagia watu tindikali, mauaji na kadhalika sasa
yanafanywa kwa kutumia bodaboda. Kama tulivyosema hapo juu, mamlaka za
udhibiti husika ziko likizo au zimelala usingizi wa pono.
Madereva hao wanadaiwa kujiundia ‘Jamhuri’
kutokana na kujiona kuwa juu ya sheria. Askari wa Barabarani wanaogopa
kuwagusa na hakuna anayehakikisha wanapata vitambulisho maalumu, usajili
wa uhakika na uratibu wa karibu wa biashara hiyo, ikiwa ni pamoja na
bodaboda hizo kupewa namba maalumu na kupakwa rangi kufuatana na
manispaa au wilaya zilikosajiliwa.
No comments:
Post a Comment