WOTE tufumbe macho na tunajaribu kutumia akili ya kawaida tu. Ni kiasi gani cha pesa timu huwa inapoteza inapoleta wachezaji wa kigeni kwa ajili ya majaribio? Hauwezi kuiona hasara hii kirahisi rahisi.
Lakini jaribu kufikiri. Analetwa mchezaji wa
kwanza kutoka Uganda. Anatumiwa tiketi ya kwenda na kurudi. Anawekwa
hotelini. Analishwa chakula. Anapewa na pesa ya matumizi kwa siku.
Jumla ya gharama zote inaangukia dola 4,000. Hapo
bado timu haijangia mkataba na mchezaji mwenyewe. Baadaye anapelekwa
mazoezini. Anafunikwa na yosso wetu waliozaliwa na kukulia Temeke na
Mkuranga.
Baada ya siku chache anatua staa mwingine feki.
Katika vichwa vya habari anakaa kurasa za mbele. Huyu naye kalipiwa
tiketi ya kuja na kurudi. Kawekwa hotelini. Analipiwa chakula na anapewa
posho kwa fedha za kigeni. Ukijumlisha gharama zote unapata Dola 4,000
nyingine.
Baada ya hapo anaenda zake mazoezini. Siku ya
kwanza mashabiki wanaguna. Siku ya pili wanaguna na wanaanza kupiga
kelele kwa jinsi anavyoshindwa kumiliki mpira vema. Siku ya tatu
mashabiki wanamzomea na kuuambia uongozi usimchukue.
Siku ya nne unakutana naye Uwanja wa Ndege
anaondoka. Hapo hapo Uwanja wa Ndege anapishana mchezaji mwingine wa
kigeni kaenda kupokewa kwa mbwembwe na viongozi. Naye hadithi inakuwa
ile ile tu.
Ukipiga hesabu hapo, klabu au mfuko wa tajiri
umepoteza dola 10,000 hata kama haukutoa noti za mkataba wa wachezaji
husika. Hizi ni gharama za malazi, chakula, tiketi za ndege. Unajiuliza,
hivi kweli sisi tuna akili?
Gharama za Dola 10,000 zinatosha kabisa kumkatia
tiketi mtu mwenye upeo akaenda kukaa nchi moja kati ya Nigeria, Ghana,
Ivory Coast au Kenya kwa wiki mbili akitazama kwa makini timu nzuri za
timu hiyo zikiwa katika mazoezi na mechi.
Hapo atatulia na kufanya kitu kinachoitwa uskauti
kwa umakini mkubwa. Mtu huyu ataambiwa kuwa timu yetu inahitaji beki,
mshambuliaji au kiungo. Ataifanya kazi kwa utulivu na kupata wachezaji
anaowataka kwa utulivu mkubwa bila ya wachezaji wenyewe kujua kama
wanafuatiliwa.
Kitu hiki inabidi kifanyike mapema wakati ligi zao
zinaendelea. Pia kinaweza kufanyika wakati ligi yetu inaendelea kwa
sababu unakuwa unajua matatizo ya timu na unajua mapema namna ya
kuyakabili pindi tu ligi inapoisha. Unaweza kumsajili mchezaji
unayemtaka kabla hata ligi yao haijaisha na wala ligi yetu haijaisha.
Hivi ndivyo wenzetu wanavyofanya. Lakini tatizo
letu tunafanya usajili wakati ligi imeisha. Tunafanya usajii wakati wa
usajili bila ya kuskauti. Ndio maana anakuja mshambuliaji mara mgonjwa,
mwingine hana uwezo kaletwa na wajanja wa mjini wanaosaka fedha.
Mwisho wa siku klabu inatumia pesa nyingi katika
majaribio bila ya kujijua ikiingia gharama za tiketi na mengineyo,
wakati ingeweza kumtuma mtu makini wakati ligi za wenzetu zinaendelea
akaangalie wachezaji wa ukweli kuliko hawa wa asilimia 10 wanaokuja.
Mchezaji mzuri hawezi kuja kwa ajili ya majaribio. Mchezaji mzuri anatafutwa alipo, anaanza maongezi wakati ligi yao wala yetu hazijaisha. Anasaini mkataba. Timu yake inapewa pesa. Ligi ikiisha anakuja kwa ajili ya msimu mpya wa mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na sio kuja kujaribiwa.
Mchezaji mzuri hawezi kuja kwa ajili ya majaribio. Mchezaji mzuri anatafutwa alipo, anaanza maongezi wakati ligi yao wala yetu hazijaisha. Anasaini mkataba. Timu yake inapewa pesa. Ligi ikiisha anakuja kwa ajili ya msimu mpya wa mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na sio kuja kujaribiwa.
No comments:
Post a Comment