
Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alipigilia msumari sakata la wabunge kuchukua posho bila kuzifanyia kazi stahiki kwa kuwaamuru wazirudishe.
Spika alitoa kauli hiyo jana asubuhi wakati akitoa
mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David
Silinde akitaka ufafanuzi wa hatua ya Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM),
Erasto Zambi kutumia Bunge kujitetea kuhusu tuhuma za kuchukua posho za
safari bila kusafiri.
Alisema Zambi ni mbunge ,pia ni Mwenyekiti wa CCM
wa Mkoa wa Mbeya na Kamishna wa Bunge anayefahamu taratibu za safari
zinazoeleza kuwa kuchukua fedha bila kwenda safari ni makosa.
Silinde wakati akiomba mwongozo huo alimtuhumu
Zambi kuwa alichukua kiasi cha Sh13 milioni za posho ya safari ya Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na nyingine kwa ajili ya safari ya
shughuli za michezo lakini hakusafiri.
“Mtu anapozungumza kwa kutumia Bunge lako
kujitetea kwa kukiuka taratibu, inaruhusiwa?” alihoji Silinde, ambaye
pia ni Waziri kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.
Kabla ya Silinde kusimama na kuomba mwongozo,
Zambi alikuwa amepewa fursa na Spika ya kuchangia taarifa za Kamati za
Bunge za Nishati na Madini na Miundombinu zilizowasilishwa juzi.
“Jana (juzi) kulitokea maneno maneno fulani hapa
bungeni. Alisimama ndugu Silinde akasema Zambi kala hela hakusafiri,”
alisema lakini kabla hajamalizia kuzungumza Spika alimkatiza... “Naomba
hilo uliache unapoteza muda na haliwasaidii wananchi, changia mambo
mengine muhimu,” alisema Spika Makinda huku wabunge wengi ndani ya
Ukumbi wa Bunge wakipiga makofi.
Hata hivyo, Zambi aliendelea kusisitiza kuwa
taswira inayokwenda kwa wananchi ni mbaya na wameanza kumpigia simu kuwa
ameiba fedha na kusema hilo ni jambo baya analostahili kulisemea.
Alisema utaratibu uko wazi kama hujasafiri
unarudisha fedha na kusema... “Ningekuwa kiongozi wa ajabu sana kama
ningekwenda Dubai na Uingereza na kutokwenda ziara ya Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana kutoka chama kinachotawala.”
Baada ya kueleza hayo, Spika alisimama na kusema:
“Waheshimiwa wabunge nimesema kama mlichukua pesa bila safari,
mnarudisha si basi…. Wote kabisa ninawajua na ninalifanyia kazi. Wote
waliochukua pesa warudishe ndiyo utaratibu wa Serikali na ndivyo
inavyotakiwa. Wote watarudisha.”
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao
aliwataka wabunge kutumia kikao cha kupeana taarifa cha wabunge wote
kuzungumza kama kuna tatizo lolote badala ya kuumbuana ndani ya Bunge.
Moto wa posho hizo ulikolea juzi pale Mbunge wa
Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba alipoomba mwongozo wa Spika
akitaka kujua hatua ya mbunge aliyechukua fedha na kwenda safari
binafsi. Nchemba alisoma ujumbe wa simu uliokuwa ukionyesha Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe alikatisha safari ya Mbunge wa
Viti maalumu (Chadema), Joyce Mukya.
Nchemba alisema ingawa hayo ni mambo binafsi, lakini alitaka
kufahamu Ofisi ya Spika inasemaje kwa mbunge aliyetumwa kuwakilisha
Taifa halafu mtu binafsi kwa kutumia nafasi yake akamrudisha.
Kauli hiyo ilimfanya Silinde kusimama na kusema
suala hilo linataka kuchukuliwa kama propaganda za kisiasa wakati wapo
pia wabunge wa CCM waliochukua fedha bila kusafiri na kumtaja Zambi.
Wadau wawaponda wabunge
Watu wa kada mbalimbali wamewashutumu wabunge na kuwatuhumu kuwa wanashindwa kuisimamia Serikali kwa kuendekeza mambo ya posho.
Chama cha Walimu (CWT), wanasiasa, wasomi na
wanaharakati hao walisema jana kwamba wabunge hao wanatakiwa kuchukuliwa
hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kujiwajibisha wenyewe au
kuwajibishwa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk
Honest Ngowi alisema: “Wabunge wanapotengewa fedha kwa ajili ya kufanya
shughuli fulani na kisha kuzitumia kwa shughuli nyingine maana yake ni
kulipeleka taifa katika umaskini.”
“Kama wanafanya hivyo, msisitizo mkubwa unatakiwa
kuwekwa wakati wakifanya marejesho ya fedha walizotumia. Wanaohakiki
matumizi ya fedha hizo wanatakiwa kuwa wakali na kama itabainika kuna
fedha zimetumika ndivyo sivyo hatua kali zichukuliwe,” alisema Ngowi.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema: “Tatizo lipo
kwa wananchi maana hawajui fedha wanazopewa wabunge kama posho ni kodi
yao. Kitendo cha wabunge kutafuna fedha za posho katika shughuli zao
binafsi maana yake ni kwamba hawawezi kuisimamia Serikali katika suala
zima la matumizi ya fedha.”
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda alisema: “Bila kujali ni mbunge
kutoka chama gani, kama akibainika kuwa alitumia fedha za posho kwa
ajili ya mambo yake binafsi, hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake
kwani matumizi mabaya ya fedha ni sawa na wizi mwingine.” Mwenyekiti wa
Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema ili
kuhakikisha kuwa fedha za walipakodi zinatumika ipasavyo, inatakiwa
kuundwa asasi ambayo itakuwa ikipanga na kusimamia mishahara na posho za
viongozi na wabunge.
“Kenya wameweza kulinda matumizi ya fedha baada ya
kubadili katiba yao na kuweka kipengele kinachoeleza kuwa mishahara na
posho za wabunge na viongozi wa Serikali zitasimamiwa na asasi.
Tunatakiwa kujua posho na mishahara ya wabunge ni kiasi gani. Katika
hali ya kawaida kabisa mbunge akitafuna posho ni vigumu kuweza
kuisimamia Serikali.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam,
Dk Benson Bana alisema tatizo lililopo ni Bunge kushindwa kusimamia
ipasavyo kanuni zake za nidhamu.
“Kama Bunge lingekuwa linawachukulia hatua wabunge
kulingana na kanuni zake, sidhani kama hali hii ingetokea, wabunge
wanaofanya vitendo vya aina hii ni sawa na mafisadi wengine,” alisema Dk
Bana.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema: “Wanatakiwa kuwajibishwa au wajiwajibishe wenyewe kama itabainika wamefanya vitendo hivi. Wabunge wanatakiwa kuwa waadilifu, sasa wanapoanza kukiuka misingi ya uadilifu ni janga kubwa.”
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema: “Wanatakiwa kuwajibishwa au wajiwajibishe wenyewe kama itabainika wamefanya vitendo hivi. Wabunge wanatakiwa kuwa waadilifu, sasa wanapoanza kukiuka misingi ya uadilifu ni janga kubwa.”
No comments:
Post a Comment