
Licha ya kuwa ni siku ya huzuni kwa dunia nzima, hotuba ya Rais wa Marekani, Barack Obama imewagusa maelfu ya watu waliokuwa kwenye Uwanja wa FNB katika ibada ya kitaifa kumwaga Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Obama aliyetumia dakika 20 katika hotuba yake
iliyokuwa ikikatizwa na kelele za kumshangilia, aliwataka vijana wa
Afrika na dunia nzima kuiga maisha aliyoishi Mandela kama yeye
alivyojifunza mambo mengi kutoka kwa mzalendo huyo.
“Miaka 30 iliyopita nikiwa mwanafunzi, nilisoma
Kitabu cha Mandela na tangu siku hiyo nilijifunza, nikajenga roho ya
uthabiti. Iliamsha uwajibikaji kwa ajili yangu na kwa ajili ya watu
wangu... hakika Mandela amenifanya niwe hivi nilivyo leo. Michelle na
mimi tumenufaika sana na Mandela,” alisema Obama na kuongeza:
“Mandela alinifanya niwe mtu ninayesimama mbele
yenu leo, alichangia kunifanya kuwa kiongozi bora. Nitaendelea kuiga
mfano wake,”
Katika sherehe hizo, Obama alipokewa kwa shangwe
na kushangiliwa kila alipopita na kila alipozungumza tofauti na
ilivyokuwa kwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma ambaye alikuwa akizomewa.
Obama alimtaja Mandela kama kiongozi anayefaa
kuigwa kwani pamoja na kukaa gerezani kwa miaka 27 akipigania uhuru,
hakutaka kung’ang’ania madaraka na badala yake alistaafu kwa hiari yake,
tofauti na viongozi wengi wa Afrika.
“Mandela alionyesha uongozi wa vitendo na
kujaribu, alikuwa ni mwanamume, binadamu wa kawaida, mume, baba na
kiongozi shupavu,” alisema Obama.
Pia Obama alisema, Mandela aliachiwa huru kama
mfungwa, lakini kama mwalimu ambaye alitumika kutuonyesha kuwa, ni
lazima kuwaamini wenzako ili nao wakuamini.
“Kufundisha upatanisho, hakuhitaji kudharau
historia mbaya ya nyuma bali ni kuikabili kwa umakini, ukweli na
uhalisia wake. Mandela alibadili sheria, lakini alibadili mioyo yetu
pia,” alisema.
Katika risala hiyo, Obama alimtaja Mandela kama
mwanamapinduzi mkubwa wa karne ya 20 aliyeibadilisha mioyo ya watu wake,
akaimarisha mapatano na maelewano kwa wazungu na weusi.
“Amezaliwa kipindi cha Vita Kuu ya Kwanza ya
Dunia, kijana aliyekuwa akichunga ng’ombe na kuteswa na wakubwa zake wa
kikabila, lakini ameibuka na kuwa mwanamapinduzi mkuu wa karne ya 20,”
alisema Obama.
Vilevile, Obama alimfananisha Mandela na Abraham
Lincoln, Rais wa zamani wa Marekani kwa kuiunganisha nchi yake pale
ilipokuwa inataka kuvurugika.
Rais huyo aliufanya umati katika uwanja huo ulipuke zaidi kwa
furaha baada ya kuzungumza neno la Kizulu, ‘ubuntu’ linalomaanisha utu
au ubinadamu ambapo alisema Mandela ameimarisha utu na ubinadamu kwa
Waafrika Kusini.
“Alidumisha ‘utu’ miongoni mwetu. Utu ambao
tunaweza kuupata kwa kushirikiana na kuwajali wanaotuzunguka,” alisema
Rais huyo ambaye anatajwa kuwa Rais wa dunia. Obama alionyesha umahiri
wake katika risala hiyo na katika sehemu ya risala hiyo alisema ni
wajibu wa kila mmoja kuiga maisha aliyoishi Mandela.
“Ni lazima tujifunze kutoka kwake, kwa sababu Waafrika Kusini kwa jumla wao wameonyesha kuwa, tunaweza kubadilika.”
Obama alimtaja Mandela kama mtu asiyependa
kujikweza bali aliyeshiriki kuonyesha mawazo yake na hofu na uhalisia
wake hasa kwa kusema kuwa yeye si mtakatifu labda kama mtakatifu ni sawa
na mwenye dhambi ambaye hachoki kujaribu. Kiongozi huyo alimalizia
hotuba hiyo kwa nukuu muhimu za Mandela zinazosema kuwa, ‘Mimi ni
kiongozi wa imani, mustakabali wangu, na mimi ni nahodha wa roho yangu’
na kuwataka Waafrika Kusini kuishi katika maneno hayo ya Mandela katika
maisha yao.
“Hakika ilikuwa roho ya ajabu, tutamkumbuka sana.
Mungu wabariki Waafrika Kusini,” alimaliza Obama. Kabla ya hotuba hiyo,
Obama alifanya jambo la kihistoria kwa kupeana mikono na Rais wa Cuba,
Raul Castro, kama ishara ya mapatano baada ya migogoro iliyoko baina ya
nchi hizo mbili.
Kabla ya Obama kuzungumza, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Ban Ki-Moon katika hotuba yake alisema kuwa, alijitoa muhanga
kwa ajili ya usalama, uhuru na demokrasia ya nchi yake.
“Sherehe hizi za kumbukumbu zinadhihirisha upinde
wa mvua wa taifa. Ninatumaini tutaweza kuuona upinde huo punde, kupitia
mvua ya simanzi,” alisema Ki-Moon. Ki-Moon alimtaja Mandela kuwa ni
kiongozi aliyejiandaa kupoteza kila kitu kwa ajili ya uhuru na
demokrasia.
“Dunia imepoteza rafiki na mwalimu. Alikuwa ni
zaidi ya viongozi wakubwa wa nyakati zetu; mwalimu mkuu aliyetufundisha
kwa mifano,” alisema Ki-Moon.
Wakati huo huo, Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo,
Jenerali Thanduxolo Mandela kwa niaba ya familia ya Mandela alipata
nafasi ya kutoa risala yake kwa Rais huyo na alisema kuwa, familia hiyo
ina bahati ya kuwa na mzazi kama Mandela.
“Utakumbukwa daima, hatuwezi kuusahau mchango wako katika familia na katika maisha ya Waafrika Kusini wote,” alisema Thanduxolo.
Baada ya Thanduxolo, walikuja wajukuu na vitukuu
wa Mandela kwa niaba ya wajukuu wote, Pumla, Andile na Mbuso Mandela
ambao walisema wana mengi waliyojifunza kwa babu yao ambaye walimtaja
kuwa kioo cha familia na kuahidi kuwa wataishi na matendo yake.
Mandela atazikwa Jumapili.
No comments:
Post a Comment