Blogger Widgets

Monday, 16 December 2013

Mengi: Sikuwahi kuomba upendeleo vitalu vya gesi


Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema hajawahi kuomba upendeleo wa kupewa vitalu vya gesi na kwamba, siku zote anapigania masilahi ya Watanzania.
Mengi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokutana na waandishi wa habari kujibu baadhi ya maelezo ambayo kwa nyakati tofauti Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyatoa.
“Mwanzoni mwa Septemba, Prof Muhongo alinukuliwa na vyombo va habari akisema: “Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali wa vitalu vya rasilimali zetu. Waelezeni Watanzania ukweli huu.”
Ukweli ni kwamba, mimi siyo mbinafsi na pili sijawahi kuomba upendeleo wa kupewa kitalu cha gesi bali ninapigania Watanzania kwa jumla,” alisema Mengi.
Alisema pia kuwa, hamiliki migodi mingi ya madini kama inavyodaiwa “Ukweli ni kwamba, mimi namiliki kwa ubia na Watanzania wenzangu mgodi mmoja wa uchimbaji wa madini ya Tanzanite wenye eneo lisilofikia hata kilomita moja ya mraba,” alisema Mengi.
Alisema kuwa, ameshapata nafasi kubwa ya kujiendeleza kibiashara na kwamba anachofanya sasa ni kupigania Watanzania wengine waweze kushiriki kama ilivyo kwenye Sheria ya Taifa ya Uwekezaji Kiuchumi ya mwaka 2004.
Sheria hii pamoja na mambo mengine, inatoa upendeleo maalumu kwa Watanzania katika rasilimali zao.
Alisema ana matumaini kuwa mkutano ambao Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuufanya leo na watu wa sekta binafsi, utasaidia kupata mwafaka wa kuwawezesha Watanzania kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi.

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf