
Siku 23 baada ya Nelson Mandela kuachiwa huru kutoka gerezani, Februari 11, 1990 aliwasili hapa nchini kwa ziara fupi iliyokuwa na msisimko wa aina yake.
Aliwasili nchini Machi 5, 1990 na kulakiwa kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (Sasa Uwanja wa Julius
Nyerere) na Mwalimu Nyerere.
Baada ya kuwasili, alikagua gwaride kama ilivyo
kawaida, lakini kikubwa ilikuwa ni hamasa ya Watanzania hasa wakazi wa
Dar es Salaam na vitongoji vyake, maelfu kwa maelfu kujipanga barabarani
kumlaki kiongozi huyo katika njia zote alizopita kuanzia Uwanja wa
Ndege.
Pamoja na mvua za masika zilizokuwa zinanyesha, hakuna aliyejali hali hiyo. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumwona Mandela.
Ilielezwa kuwa Mandela na ujumbe wake angewasili
mapema zaidi, saa 4:00 asubuhi, lakini ratiba ilibadilika kuwa
angewasili saa 11 jioni, lakini watu hawakupungua barabarani,
walijipanga mapema kuanzia Uwanja wa Ndege, Barabara ya Pugu (sasa
Nyerere) na maeneo mengine kumlaki mpigania uhuru huyo.
Wakati huo Dar es Salaam ilikuwa na tatizo kubwa
la usafiri, lakini hakuna aliyejali. Mara baada ya Mandela kutua,
ilinyesha mvua kubwa, watu walikubali kulowa lakini hadi wamwone
Mandela.
Mandela alipata mapokezi makubwa na ya aina yake
jijini Dar es Salaam. Kikubwa ni kwamba, Mandela alikuwa akizungumzwa
sana na vyombo vya habari, kuonwa kwenye magazeti lakini wengi walitaka
kumwona Mandela na mkewe Winnie uso kwa uso.
Baada ya shughuli za Uwanja wa Ndege kukamilika na
mvua kukatika, Mandela aliyefuatana na mkewe, Winnie walipanda gari ya
wazi aina ya Rolls Royce wakiwa na Mwalimu Nyerere kwa pembeni.
Maelfu kwa maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam
walijipanga kuanzia Uwanja wa Ndege, Barabara ya Pugu, Uhuru, Kariakoo,
Stesheni, Luthuli hadi Ikulu na watu wote hao walikuwa na shauku ya
kumuona Mandela walitimiza kiu yao. Kila mmoja alifurahi baada ya
kumuona Mandela aliyekuwa akipunga mkono muda wote.
“Ndoto yangu imetimia”, “Siamini, nimemwona
Mandela?”, “Safi”, “Naweza kufa kwa amani...nimemwona Mandela” zilikuwa
kauli za watu mbalimbali waliokuwa wamejipanga barabarani kumlaki
Mandela akiwa na Winnie walipokuwa wakipita.
Siku iliyofuata, hali ilikuwa zaidi ya siku ya
mapokezi. Watu waliombwa kufika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa
Uhuru) na ilikuwa mminyano wa aina yake. Zaidi ya watu 100,000
wanasadikiwa walifurika uwanjani kusikiliza hotuba ya pili ya Mandela
tangu atoke gerezani.
Mandela alitoa hotuba ya kwanza akiwa City Hall
nchini Afrika Kusini. Aliwahutubia wafuasi wa ANC wapatao 50,000
waliokuwa wakimsubiri kwa hamu kumuona baada ya kifungo cha miaka 27
jela, ambako pamoja na yote alionyesha furaha yake kulakiwa na maelfu ya
wapenzi na wafuasi wake hao.
Mwalimu Nyerere akiwa na mgeni wake, alianza kumpongeza Mandela
kwa kuwa ni kati ya watu wanaostahili heshima kutokana na mapambano yake
dhidi ya siasa dhalimu ya makaburu wa Afrika Kusini. Makaburu
walikithiri kwa siasa zao za kibaguzi.
Alisema kuwa kujitokeza kwa watu wengi kiasi hicho
ilikuwa inadhihirisha kuwa Mandela anagusa akili za watu wengi kutokana
na mapambano ya kumtetea mtu mweusi.
Kutokana na mchango wake wa kupigania haki na
uhuru, Mwalimu Nyerere alimtunukia Mandela, Nishani ya Kilimanjaro
Daraja la Pili ambayo mara nyingi hupewa Mawaziri Wakuu na viongozi
wengine wenye kariba kama ya Mandela.
Akihutubia maelfu ya Watanzania na sauti yake nzito, Mandela alionyesha furaha yake kwa mapokezi makubwa ya Watanzania.
Pia Mandela alitumia nafasi hiyo kuwashukuru
Watanzania kwa kukiunga mkono chama chake cha ANC katika mapambano ya
ukombozi dhidi ya ubaguzi na utawala dhalimu wa makaburu.
Ziara ya Zanzibar
Machi 7, 1990 ujumbe wa Mandela ulikwenda Zanzibar
ambako pia shughuli mbalimbali zikiwamo za biashara zilisimama kwa
takribani saa nne, huku kila mmoja akiwa na shauku ya kumuona Mandela.
Mbali na kufurika mitaani, Uwanja wa Ndege ulikuwa
umefurika pamoja na Uwanja wa Uwanja wa Amaan, Wazanzibar walijaa
kumlaki ‘Comrade’ Mandela.
Neno ‘Amandla’ lilisikika kutoka kwa waliofika
kumlaki Mandela aliyekuwa amepakizwa kwenye gari aina ya Landrover
kwenda uwanjani.
Itakumbukwa, kwa mara ya kwanza, Mandela na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume, walikutana Addis Ababa mwaka 1962.
Mandela aliyetembelea Tanzania kwa mara ya kwanza
katika ziara fupi mwaka 1962, alipofika Zanzibar baada ya kutoka
gerezani, aliomba apelekwe kwenye Kaburi la Karume pamoja na eneo ambalo
Rais Karume aliuawa.
Kati ya vitu alivyovizungumza akiwa Zanzibar,
alisifu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kwamba viongozi wa Afrika
wanaosaka umoja, wajifunze muundo huo wa Muungano kutoka Tanzania.
Naye Winnie alisema kuwa atakaporudi Soweto atawasimulia Waafrika Kusini jinsi walivyopokewa vizuri, na kuwaeleza ukarimu walionao Watanzania.
Naye Winnie alisema kuwa atakaporudi Soweto atawasimulia Waafrika Kusini jinsi walivyopokewa vizuri, na kuwaeleza ukarimu walionao Watanzania.
No comments:
Post a Comment