
Ili kuziwezesha kupata rejea za masomo na kuingia kwenye mfumo wa taarifa za kitaaluma.
Dar es Salaam. Zaidi ya taasisi
120 za elimu ya juu na utafiti zinafungwa vifaa vya mtandao
vitakavyoviunganisha na Mkongo wa Taifa ili kuziwezesha kupata rejea za
masomo wanayochukua, mawasiliano na kuingia kwenye mfumo wa taarifa za
kitaaluma za ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Wizara
ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba wakati akipokea
vifaa vya mradi wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu vitakavyofungwa
awamu ya kwanza katika taasisi 28 kwa kuziunganisha kwenye Mkongo wa
Taifa.
Makamba alisema mradi huo unafadhiliwa na Benki ya
Dunia iliyoikopesha Serikali Dola 100 milioni kwa ajili ya kuutekeleza.
Mkandarasi M/S Softnet Technologies Ltd Tazania ndiye aliyepewa kazi ya
kufunga vifaa hivyo.
“Katika kipindi cha Desemba na Februari mwakani
vifaa vyenye thamani ya Dola 2.2 milioni vitakuwa tayari vimefungwa
katika taasisi 28 na kuanza kutumika,” alisema Makamba.
Awamu ya kwanza vyuo vya elimu ya juu
vitakavyounganishwa ni kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Arusha
Mbeya, Kilimanjaro, Morogoro na Zanzibar, likiwamo Baraza la Mitihani
Tanzania (NECTA).
Lengo ni kusaidia kuondoa gharama za mawasiliano
vyuoni, kukabiliana na changamoto ya wahadhiri kwa kuwa mhadhiri mmoja
atafundisha vyuo zaidi ya 20 kwa kutumia vifaa hivyo vya sayansi na
teknolojia na rejea zote zitakuwemo ndani ya maktaba ya mtandao huo za
ndani na nje ya nchi, chuo kimoja kitawasiliana na kingine bure bila ya
kuwepo gharama.
“Elimu ya juu inategemea kupata manufaa toka
maktaba, mradi huu utawawezesha wanafunzi kupata vitabu na taarifa
kutoka chuo chochote duniani. Lakini natoa wito kwa wanafunzi na
wanaoongoza taasisi za elimu nchini kuvithamini na kuvitunza na
kuvitumia kwa manufaa mengine.”
No comments:
Post a Comment