Blogger Widgets

Saturday, 23 November 2013

Uhondo: Kikosi bora kinachokosa fainali za Kombe la Dunia Brazil 2014

 
MAJINA yaliyotua Brazil kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia yanatia raha. Vigogo wote watakuwa kwenye fainali hizo, ikiwamo washindi wote wa fainali 18 zilizopita. Maandalizi yote yamekamilika hasa katika mji wa Sao Paulo utakaokata utepe wa fainali hizo Juni 12 mwakani.
Vikosi 32 vitakavyoundwa na mastaa watupu vitajipanga kuishtua Dunia. Itakuwa ni vita iliyojitosheleza. Nchi nane zilizokuwa zimekosa fainali zilizopita kule Afrika Kusini zitakuwapo Brazil mwakani.  Colombia, Ecuador na Costa Rica zimerudi upande wa Amerika Kusini, wakati Ulaya, Mtaliano Fabio Capello ataiongoza Urusi, kiungo Luka Modric atakuwa na Croatia na Bosnia itashiriki kwa mara ya kwanza. Ubelgiji nayo itarejea katika anga hilo. Wengineo, Iran wataongeza uhondo.
Cristiano Ronaldo atakuwapo, Lionel Messi pia. Hapo usiwataje Andres Iniesta na Xavi, Radamel Falcao, Alexis Sánchez na Arturo Vidal, Luis Suarez na Edinson Cavani, Mesut Ozil, Eden Hazard, Robin Van Persie na Arjen Robben, Wayne Rooney, Mario Balotelli, Franck Ribery na Karim Benzema watakaokuwapo pia.
Hapo hujataja wakali wa Afrika kina Yaya Toure, Kevin Prince Boateng, Didier Drogba na John Obi Mikel, Asamoah Gyan, Gervinho, Salomon Kalou, Emmanuel Emenike, Alex Song na Samuel Eto’o. Droo ya makundi itafanyika Desemba 6 mwaka huu na baada ya hapo kutakuwa na miezi sita kwa timu 31 kuanza mchakato wa kuivua taji Hispania.
Hata hivyo, wakati ukifurahia majina yote makubwa utakayotarajia kuyaona katika fainali hizo, kuna mastaa wengi tu watakosekana ambao wanaweza kuunda kikosi ambacho kinaweza hata kunyakua taji hilo. Hiki ndicho kikosi cha kwanza bora kabisa (Best Eleven) cha mastaa watakaokosa fainali hizo za Brazil mwakani.
Kipa:
Petr Cech (Czech)
Kipa huyo mzoefu wa Chelsea inawezekana hayupo kwenye ubora wake kwa sasa, lakini bado anabaki kuwa kipa mahiri kwa takriban muongo mmoja sasa kwenye klabu yake na timu ya taifa.
Ni kiongozi wa kweli ndani na nje ya uwanja. Cech analimiliki vyema eneo lake la kiuchezaji licha ya kuwa alipata majeraha makubwa mwanzoni mwa soka lake.
Alionyesha ubora wake kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 alipodaka mkwaju wa penalti, kabla ya kumgomea pia straika wa Liverpool wakati huo, Andy Carroll, kwenye fainali ya Kombe la FA mwaka 2011 na aliokoa pia mkwaju wa Javier Hernandez wa Manchester United mapema mwaka huu. Kwa kifupi tu huyu ni kipa bora ambaye hatakuwapo Brazil mwakani.
Beki wa Kulia: 
Branislav Ivanovic (Serbia)
Kwenye namba hiyo, beki huyo mwenye nguvu amemshinda mwenzake wa Poland, Lukas Piszczek. Ivanovic ni mahiri kwa soka la aina zote, juu, chini na anaweza kujiweka kwenye nafasi yake. Ni chaguo bora kwenye beki ya kulia, pia anaweza kucheza kama beki wa kati akiwa tishio pia anapopanda kushambulia.
Beki wa Kati:
Mehdi Benatia (Morocco)
Ni mmoja wa mabeki bora wanaotesa Ulaya msimu huu akiwa na kikosi cha AS Roma. Ukitazama idadi ya mabao machache iliyoruhusu Roma hiyo ni kazi ya Mmorocco huyo ambaye hatakuwapo Brazil mwakani.
Benatia ni kiboko ya mastraika wote wajanja wajanja, ni beki anayetumia akili sana anapokuwa uwanjani na ndio maana AS Roma inayonolewa na Rudi Garcia imeruhusu mabao matatu tu katika mechi 12 za Serie A msimu huu.
Beki wa Kati:
Daniel Agger (Denmark)
Beki huyo wa Liverpool ni fundi mzuri wa kutumia mguu wa kushoto, kwa kipindi chote alichodumu Anfield anatajwa kuwa mmoja wa mabeki bora kwenye Ligi Kuu England licha ya sasa kuwekwa kando.
Alikuwa mhimili imara kwenye kikosi cha Denmark kilichomaliza kikiwa cha pili kwenye kundi lake la kufuzu fainali za Kombe la Dunia za Brazil, lakini kwa bahati mbaya hawakuwamo kwenye mchujo.
Beki wa Kushoto:
David Alaba (Austria)

Staa wa Bayern Munich ambaye ni hatari sana kwa sasa. Ni mchezaji kiraka anayewapa fursa nyingi miamba hiyo ya Ujerumani. Anapokuwa upande wa kushoto, kasi yake imekuwa na faida kubwa kwa Bayern Munich licha ya taifa lake kumtumia katika nafasi ya kiungo.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya hawakuweza kushindana na timu za Sweden na Ujerumani kwenye kundi lao na hivyo wanasubiri kujaribu bahati kwenye Euro 2016.
Kiungo wa Kati:
Marek Hamsik (Slovakia)
Kiungo fundi wa ndani ya uwanja. Ana macho ya uhakika, pasi za hatari na amekuwa akichezesha mpira wake uwanja mzima jambo linalomfanya kuwa mmoja wa viungo bora kabisa kwa sasa.
Kwenye kikosi cha Napoli, kocha Rafa Benitez, anamtumia katika namba 10 ambapo anacheza mbele ya viungo, Gokhan Inler na Valon Behrami, huku akiwa sambamba na straika Gonzalo Higuain.
Kwa bahati mbaya taifa lake halikuweza kushindana na timu za Bosnia na Ugiriki na hivyo kumaliza kwenye kundi lao wakiwa na pointi 13 tu baada ya mechi 10.
Kiungo wa Kati:
Aaron Ramsey (Wales)
Kwa zaidi ya miezi minane iliyopita, kiungo huyo wa Arsenal ameliteka soka kwenye miguu yake. Ameonyesha kila aina ya ufundi na kumsaidia Arsene Wenger kupata pointi muhimu zinazomfanya aongoze Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, kwenye kufuzu fainali za Kombe la Dunia mambo hayakuwa mazuri na kikosi chake cha Wales kilimaliza nafasi ya tano kati ya timu sita zilizokuwa zikiunda kundi lao. Lakini kwa kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, Ramsey yupo kwenye ubora mkubwa na ni mchezaji staa atakayezikosa fainali hizo.
Kiungo wa kulia: 
Gareth Bale (Wales)
Ni mchezaji mwenye kasi, nguvu na ufundi mkubwa, jambo ambalo linatosha kumtambulisha staa huyo wa Real Madrid. Baada ya kuanza vibaya kwenye timu yake mpya kufuatia usajili wa Pauni 85 milioni, Bale kwa sasa amerejea katika ubora wake na kuwa tishio, lakini sasa kwa bahati mbaya hatakuwapo mwakani kwenye fainali za Kombe la Dunia na tumaini lililopo kwake ni kujaribu nafasi ya kucheza Euro 2016.
Kiungo wa kushoto:
Arda Turan (Uturuki)
Ni kiungo mwenye kipaji cha maana kutoka Uturuki. Amekuwa akifanya makubwa katika kila timu anayochezea kabla ya kujiunga na Atletico Madrid chini ya Diego Simeone.
Tangu alipojiunga na Muargentina huyo, Turan amekuwa kwenye ubora mkubwa na angekuwa mmoja wa wachezaji kivutio kama angekuwapo Brazil mwakani.
Fowadi:
Zlatan Ibrahimovic (Sweden)
Baada ya kipigo kutoka kwa Cristiano Ronaldo, aliyeiwezesha Ureno kufuzu fainali za Kombe la Dunia baada ya kucheza mechi ya mchujo dhidi ya Sweden, mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic sasa hatakuwapo kwenye fainali hizo.
Licha kwamba alifunga mara mbili Jumanne iliyopita, jambo hilo halikumsaidia kupata tiketi ya ushiriki wa fainali hizo na sasa Ibracadabra hatakuwapo Brazil.
Straika:
Robert Lewandowski (Poland)
Hakuna ubishi kwamba ndiye Namba 9 hatari Ulaya kwa sasa baada ya msimu uliopita kufunga mabao 36 na msimu huu akiendelea kuwa silaha hatari ya Borussia Dortmund akiwa amefunga mabao 13 katika mechi 19.
Straika huyo ni mahiri wa kuwasoma mabeki na kutumia udhaifu wao kwa umakini mkubwa jambo linalomfanya kocha, Jurgen Klopp,  kunufaika kwa huduma yake kwenye Bundesliga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya Lewandowski ameshindwa kuivusha Poland kwenda fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil na jambo hilo linamfanya kuwa mmoja wa mastraika mahiri kabisa duniani watakaokosa michuano hiyo.
Benchi la akiba
Kikosi hicho kitatumia mfumo wa 4-4-2 na hakika kama kingepelekwa kushiriki fainali hizo basi ungetarajia kuwaona kwenye hatua ya kuanzia robo fainali na hilo lingetokana na kuwa na timu ya nguvu huku kwenye benchi lao la akiwa kukiwa na mastaa kama Papiss Cisse (Senegal), Christian Eriksen (Denmark), Martin Skrtel (Slovakia), Andriy Yarmolenko (Ukraine), Lukas Piszczek (Poland), Samir Handanovic (Slovenia) na Jefferson Farfan (Peru).

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf