
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimemtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi ya Lugha, Profesa Ngugi wa Thiong’o kutokana na mchango wake mkubwa kwa Bara la Afrika katika kujikomboa kiakili dhidi ya ubeberu wa lugha za kigeni.
Ngugi ambaye ni nguli wa fasihi za lugha na pia ni
mhadhiri katika Chuo Kikuu cha California huko Marekani, alitunukiwa
shahada hiyo jana, Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya 43 ya UDSM.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala,
alisema chuo kimeamua kumpa shahada hiyo kutokana na mchango wake wa
kupinga chuki na dharau zinazofanywa na mataifa ya Ulaya dhidi ya lugha
za Afrika.
“Katika jitihada hizo, Chuo Kikuu kimeruhusu
tasnifu (Thesis) za Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili
ziwasilishwe katika Lugha ya Kiswahili. Pia Chuo kinasisitiza kuwa
tasnifu zote hapa chuoni ziwe na muhtasari mfupi ulioandikwa kwa
Kiswahili,” alisema.
Akishukuru baada ya kukabidhiwa shahada hiyo ,
Ngugi alisema hiyo ni shahada yake ya nane kutunukiwa na vyuo mbalimbali
duniani na ya pili kwa Afrika.
No comments:
Post a Comment