
Kwa msaada wa gazeti la mwananchi
Aliyekuwa Mbunge wa Songea mjini kuanzia Oktoba 1985 hadi Aprili 1988 alipofungwa jela miaka 11, Abdulrabi Ali Yusuph (66), amesema tangu atoke gerezani hadi sasa anaomba aonane na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ama Rais Benjamin Mkapa na hata Rais Jakaya Kikwete lakini hajafanikiwa hadi leo.
Amesema aliomba nafasi ya kumwona Rais Mwinyi
akiwa madarakani ili amweleze ya moyoni, lakini hakufanikiwa na
aliendelea kuomba amwone Rais Mkapa hakufanikiwa na sasa anaomba amwone
Rais Kikwete bado hajajaaliwa.
Alisema hayo katika mahojiano maalumu
yaliyofanyika nyumbani kwake Mtaa wa Mfaranyaki mjini Songea ambako
anaishi akiwa kwenye nyumba chakavu ya urithi na wake zake wawili pamoja
na watoto kadhaa.
Mahojiano ya mwandishi na mbunge huyo yalianza hivi.
Mwandishi: Mheshimiwa habari za
siku nyingi. Nimefika hapa kwa niaba ya jarida la Ndani ya Habari
linalochapishwa na gazeti la Mwananchi, lengo hasa ni kukujulia hali.
Watu wangependa kujua unaendeleaje hasa baada ya kifungo chako.
Ningependa kupata maelezo yako juu ya masuala ya maisha ya gerezani na
ya sasa ukiwa huru.
Mbunge. Kwanza kabla ya yote. Wewe upo hapa ili uuze gazeti na upate fedha. Je, mimi unanieleza vipi kuhusu mapato hayo.
Mwandishi: Kazi ya mwandishi
siyo biashara, bali ni ya kijamii. Kazi ya mwandishi ni kuelimisha,
kufundisha, kuibua kero na kutaarifu jamii. Kazi ya mwandishi inaweza
kukusaidia ama kukuharibia kwa kuibua mambo ambayo unaweza kufanya kwa
kuvunja sheria na kuitisha jamii.
Mbunge: Kwa maneno yako haya ni kwamba mimi sina lolote la kufaidika leo?
Mwandishi: Ni kweli sikuja hapa
kibiashara bali kukusalimu na kupata hisia zako ama kauli yako baada ya
kufungwa jela kwa miaka 11 ukiwa mbunge na sasa upo nje, hivyo
tunapenda kujua uliishi vipi jela na jamii inakuonaje baada ya kutoka?
Mbunge:Basi kwa kuwa umefika
hapa, nitasema machache, lakini kama utakuja baada ya kujipanga,
nitaeleza mengi mno. Mimi ninazo kero na mambo mengi baada ya kuishi
gerezani na kwa kweli nina masikitiko mengi ambayo yananisononesha sana.
Mwandishi:Nashukuru Mheshimiwa, naomba udokeze hisia zako walau kidogo.
Mbunge: Kwanza ninayo masikitiko
mpaka leo kwa viongozi wakuu wa taifa hili. Nasikitika mpaka leo kwa
kunyimwa nafasi ya kuonana na walau mmoja kuanzia Rais wa awamu ya
pili, Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na hata awamu ya
nne Jakaya Kikwete.
Mimi ninayo mambo mengi sana kwa viongozi wetu, Serikali na hata
kwa taifa, lakini nasikitika kuona waliokuwa viongozi wenzangu
wamenitenga kana kwamba mimi ni shetani’’ anasema.
Mimi nilibambikiwa meno ya tembo na hatimaye
nilifungwa jela, nilichojifunza cha kwanza ni kwamba jamii ina tabia ya
kuwanyanyapaa waliowahi kufungwa jambo ambalo hata viongozi wa taifa
nao wanatekeleza kwa vitendo juu yangu. Wapo viongozi wenzangu ambao
wakati ule tulicheka pamoja, tulikula pamoja na kucheza pamoja, lakini
baada ya mimi kwenda jela hawaonekani.
Kufungwa kwangu kulipangwa
Mwandishi:Unasikitika kwa kufungwa kwako ama kunyanyapaliwa?
Mwandishi:Unasikitika kwa kufungwa kwako ama kunyanyapaliwa?
Mbunge:Mimi baada ya kufika
gerezani nilijiuliza swali la kwanini nimefungwa? Maana ukweli ni
kwamba meno ya tembo siyo yangu. Baadaye nilipata jibu kwamba nilifungwa
ili nikaone mambo maalumu magerezani. Mambo niliyoyashuhudia
yanatisha. Lakini la kwanza ni kwamba siyo wote wanaofungwa wanatenda
makosa waliyoshtakiwa nayo. Pili niligundua kwamba askari magereza si
wabaya wakiwa kazini, bali wabaya ni waliokupeleka kwao.
Pia nilijifunza kwamba askari magereza wanafanya
kazi katika mazingira magumu kiasi kwamba wanafika hatua ya kuomba
msaada kwa wafungwa. Pia niliona wazi kwamba wapo wafungwa wanaorudi
gerezani kwa kupenda huku wengine wakirudishwa gerezani kwa hila za
udhalimu.
Nilishuhudia kunyongwa kwa wafungwa 11 na
nilishiriki kusafisha vitanzi vyao, miongoni mwao, wapo walionyongwa
huku wakikana kutenda makosa waliyoshtakiwa nayo.
Mwandishi: Maisha yalikuwaje gerezani?
Mbunge:Baada ya kuhukumiwa
kufungwa nilitoka gereza la Songea kwenda gereza la Lilungu Mtwara,
baadaye nilipelekwa Ukonga Dar es Salaam na hatimaye Gereza la Maweni
Tanga. Cha kushangaza katika magereza yote mimi nilikuwa mnyapala mkuu
na pia imamu wa kuswalisha Waislam waliofungwa.
Aporwa mke baada ya kufungwa
Mwandishi:Ukiwa jela , je uliifikiriaje familia yako?
Mbunge:Kwa kweli nasema wazi
kwamba suala la kufungwa kwangu lilipangwa na watu mbalimbali. Nasema
hivi kwa sababu baada ya miezi mitano hivi , kiongozi wa dini ya
Kilokole alinifuata nikiwa Gereza la Lulindi na kuniambia kwamba mke
wangu alimbadilisha dini na kuwa mlokole na aliamua pia kumuoa.
Mpaka leo mke wangu wa kwanza ambaye nilizaa naye
watoto sita hatujarudiana na amesababisha baadhi ya watoto wangu wawe
walokole hadi leo
Mwandishi: Kwa hali hiyo huna mke mpaka sasa?
Mwandishi: Kwa hali hiyo huna mke mpaka sasa?
Mbunge. Hapana, kwa sasa nina wake wawili na watoto, watoto, eeeh nina watoto kadhaa.
Mwandishi: Ulifungwa miaka tisa
nwaka 1988 , lakini ulikata rufaa ambayo ulishindwa na hatimaye kufungwa
miaka mitatu zaidi, lakini ulitoka kwa msamaha wa Rais ikiwa imebaki
miezi minne, je ulijisikiaje?
Mbunge: Nakumbuka nilitolewa siku
ya Ijumaa. Basi nikaanza kuifikiri sana siku hiyo kuwa ina maana kubwa
kwangu. Nasema hivyo kwa sababu nilizaliwa Ijumaa, nilikamatwa kwa
tuhuma za meno ya tembo siku ya Ijumaa, nilihamishwa kutoka Songea
kwenda Lulindi siku ya Ijumaa na hatimaye kuachiwa siku ya Ijumaa. Jambo
hili lilinipa wasiwasi na kujiuliza mara kadhaa maana yake ninni.
Lakini mama yangu mzazi aliyefariki mwaka juzi nakumbuka alinisihi
nimshukuru sana Mungu kwa siku yake ya Ijumaa kuifanya kuwa ya matukio
makuu.
Mwandishi:Ukiwa gerezani kuna mambo gani unaoyakumbuka zaidi.
Mbunge: Kwa kweli nayakumbuka
yaliyokuwa yakitokea nje ya gereza juu yangu. La kwanza
linalonisikitisha sana ni taarifa ya Kiongozi wa Bunge (anamtaja jina)
ambaye aliwahi kulitangazia Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba aliyekuwa
mbunge na kufungwa jela Abdulrabi Ali Yusuph amefariki dunia.
Jambo hili lilinisikitisha sana. Nilimwambia
Marehemu Dk Laurence Gama akiwa mbunge jambo hilo kwamba nilikerwa sana
na alinihakikishia kulimaliza.
Jambo la pili lililonishtua ni kauli ya Rais wa
awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi alipotamka kwamba Serikali yake haina
upendeleo katika masuala ya dini akitoa mfano kwamba padri Erio
aliyekamatwa kwa makosa ya kuvunja sheria aliamwaachia, lakini ameamua
Muislam mwenzake akitaja jina langu aendelee kusota jela. Kauli ile
ilinihuzunisha kwa vile kwanza kosa lilikuwa la kubambikiwa na pili
kiongozi mkuu anatangaza kuniacha nisote jela.
Mwandishi: Pamoja na kwamba unasema jamii ina mwelekeo wa kuwanyanyapaa wanaofungwa, je wapiga kura wako nao walitekeleza hayo?
Mbunge: Baada ya kutoka
gerezani, wapo wana CCM waliofika na kunitaka niwe kiongozi ngazi ya
wilaya, kata na hata mtaa, lakini nilisita sana ingawa baadaye
nilikubali kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mfaranyaki hadi mwaka jana.
Kwa ujumla utendaji wa CCM kwa sasa umebadilika sana. Hauna shukrani
hata kwa waasisi wake. Mimi nina historia ndefu ya Chama hiki. Baba
yangu marehemu Abdulrabi Yusuph ndiye aliyekuwa Katibu wa kwanza wa
Chama cha TANU. Baba yangu ndiye aliyefanya kazi na Nyerere kwa dhati.
Mwandishi: Viongozi wa Serikali wanaweza kukusahau, je wale wa CCM nao?
Mbunge: Nakueleza baada ya
kufungwa, wana CCM walinisahau kabisa , lakini siku moja dada yangu
alikwenda Uwanja wa Majimaji alipotembelea Rais wa awamu ya pili Ali
Hassan Mwinyi na kumwangukia miguuni
Askari na vyombo vya usalama vilitaka kumfunga dada yangu,
lakini Rais aliagiza mwanamke huyo afike Ikulu Songea ambako alikwenda
na kuomba Serikali isaidie kuwasomesha watoto wangu wawili ambao alikuwa
akiishi nao mimi nikiwa jela.
Basi nashukuru Mwinyi aliagiza CCM iwasomeshe
watoto wawili ambao kweli walisomesha hadi kidato cha nne wakati mimi
nikiwa jela.
No comments:
Post a Comment