
SAYANSI ya soka ni kitu cha kuvutia japokuwa pia ina mkanganyiko wa aina fulani na ni vigumu kupata uwiano wa kete zake.
Kila mara vyombo vya habari vimekuwa vikizungumzia
habari za mchezaji fulani kutaka au kutakiwa kwenda klabu hii au ile,
hata kama sio msimu wa usajili.
Kumalizika kwa dirisha moja la usajili huwa
mwafaka kwa wang’amuzi wa klabu mbalimbali na mawakala kutafuta madili
kwa ajili ya wachezaji.
Tofauti na kutekeleza wajibu wao kikazi,
wanatafuta pia ‘kula’ yao na pia kujijengea wasifu, maana hatimaye
kinachowapandisha chati kama mawakala au wang’amuzi ni aina ya wachezaji
waliowanasa au kuwezesha kusajiliwa.
Hili suala la Gareth Bale kusajiliwa Real Madrid kwa Pauni 85 milioni kwa mfano, linatakiwa kutazamwa kwa jicho la tatu.
Wapo wanaojenga hoja kwamba Real Madrid imepoteza
fedha hizo au kwamba Rais Florentino Perez anataka tu sifa hapo Santiago
Bernabeu.
Nimetazama suala hili kwa upande mwingine na pia
nilipata nafasi ya kuzungumza na watu kadhaa wiki iliyopita katika
udadisi wa masuala ya soka, thamani ya wachezaji, ununuzi wao na faida
kwa klabu.
Mmoja wao ni mtu mwenye uzoefu wa muda mrefu
katika masuala ya soka, Jol Kinneear. Ameanzia kucheza, ukocha hadi
ukurugenzi wa soka.
Huyu ni raia wa Ireland aliyehamia hapa England
tangu akiwa na umri wa miaka sita na sasa amefikisha miaka 66 na anasema
maisha yake yote ni soka tu.
Alikuwa beki Tottenham Hotspurs kwa misimu 10 na baada ya hapo amekuwa kocha na sasa ni mkurugenzi wa soka.
Huyu ni mtu anayejiamini kweli kweli na alinieleza
kwamba klabu inaposajili mtu mwenye jina kubwa, haitegemei tu kwamba
atawafungia mabao, atadaka vizuri au atajenga ukuta imara au kiungo,
bali tafakari inakwenda mbali zaidi ya hapo.
Real Madrid kumsajili Bale kwa mapesa yote yale,
kwa mfano, haina maana kwamba inatarajia atikise nyavu zaidi ya wengine
wala kwamba ndiye mchezaji bora zaidi duniani.
Lakini ukweli ni kwamba kwa muda macho na masikio ya mashabiki
wa soka, makocha, mawakala, wang’amuzi, wakurugenzi wa klabu na kampuni
za matangazo yalielekezwa kwa kijana huyu aliyezaliwa Wales miaka 24
iliyopita.
Tayari Real Madrid walikuwa na mchezaji ghali
kuliko wote – Cristiano Ronaldo, lakini bado waliweka shinikizo wampate
Bale licha ya kwamba hawakuwa na mahitaji makubwa sana kwa mtu wa nafasi
yake uwanjani.
Lakini nimekuja kung’amua, kama alivyonigusia
Kinneear, Real Madrid inajijengea jina na sasa macho yote yaliyokuwa kwa
Bale, yanaunganishwa kwa Real Madrid, hapo tayari wamefanya biashara
kubwa sana na mauzo yamepanda ajabu.
Kampuni nyingi kubwa zitataka kutangaza kwenye
mabango yaliyopo Bernabeu, kwenye mtandao wa klabu hiyo na katika jezi
za wachezaji wake, maana kuna miamba miwili ghali zaidi duniani.
Hatimaye, kwa kudunduliza namna hii, klabu inaweza
kupata dili kubwa sana za biashara na pia vituo zaidi vya televisheni
vitakimbilia kurusha mechi zake.
Utafiti wangu unaonyesha kwamba Real Madrid ni
moja ya klabu mbili nchini Hispania zinazokomba pesa nyingi kutokana na
matangazo ya televisheni, ambapo tofauti na England, kule Hispania
hakuna usawa wa magawio. Klabu nyingine inayodaka kitita kikubwa ni
Barcelona.
Kitu kama hicho cha klabu kutolipwa sawa ndicho
kinapiganiwa na Liverpool hapa England, ambapo wanataka klabu kubwa
zilipwe zaidi, badala ya Manchester United, Arsenal, Chelsea, Liverpool
kulipwa fedha za matangazo sawa na Crystal Palace, Norwich, West
Bromwich Albion na nyinginezo.
Japokuwa wazo lao halijakubaliwa, nguvu ya soko
inaweza kulifanya likubalike siku zijazo. Uamuzi wa wamiliki wa klabu
hiyo, John Henry na kampuni ya Fenway Sports Group kutaka malipo kwa
kadiri ya thamani ya klabu unaonesha mantiki hii pia.
Uzuri wa wachezaji ni moja ya vigezo vya mashabiki kuzipenda, kwenda kutazama ambapo hulipa viingilio vikubwa tu hapa England.
Labda ndiyo maana Liverpool walikataa kumuuza Luis
Suarez pia ili kuhakikisha wanazidi kufanya vyema mchezoni na kupanda
chati, na tunashuhudia sasa wakienda vizuri.
Katika kujiongezea thamani pia, Liverpool wana
mkakati wa kupanua uwanja wao wa Anfield ili kuipandisha timu ngazi na
kuchuana na klabu kama Arsenal na Manchester United zinazoongoza kwa
viwanja vikubwa na mapato.
Makusanyo ya Liverpool kwa siku za mechi mwaka
2011 yalikuwa Pauni 42.9 milioni, kidogo mno ikilinganishwa na yale ya
Arsenal – Pauni 93.9 milioni au Man United iliyochuma Pauni 100.2
milioni.
Tunaona pengo kubwa hapo ambapo linatosha kununua mchezaji nyota
wa kimataifa kama Mesut Ozil labda ambaye kwenda kwake Arsenal tayari
kumeanza kuleta mabadiliko chanya dimbani lakini pia
kwenye biashara ya mali zao mbalimbali.
Liverpool imekuwa inataka kuupanua uwanja wao
lakini imebaki katika nadharia kwa muda mrefu, ambapo pamoja na kuongeza
watazamaji na mapato ya tiketi, uwanja utakuwa na hadhi zaidi hivyo
kuvutia matangazo ya kampuni mbalimbali.
Inataka kuongeza watazamani kwa asilimia 35 ili
kunyanyua mapato yake, watalii nao watapenda kwenda Liverpool kuliona
jiji lakini pia kushuhudia uwanja na kupiga picha humo na kwa ujumla
vitabu vya akaunti za klabu zitanona.
Kwa hiyo viongozi wa klabu katika ngazi mbalimbali
hukuna vichwa kila wakati kuhangaikia usajili, kutengeneza timu nzuri
yenye ufanisi dimbani, viwanja bora na kuhakikisha uwiano wa hesabu
unazipaisha klabu kiuchumi kwa ujumla ili zipate faida na si kuelekea
kufilisika.
No comments:
Post a Comment