
MAKALA Na Elias Msuya,Mwananchi
Hali inayoendelea ndani ya Chadema imezua taharuki kubwa kwa Watanzania wengi. Hiyo ni kutokana na matumaini makubwa ya chama hicho waliyoyaweka kwa wananchi.
Wengine wanasema sasa yametimia. Kwamba kama ilivyokuwa kwa NCCR Mageuzi mwishoni mwa miaka ya 1990 ndiyo yanakipata Chadema.
Kwangu mimi naona haya ni majaribu tu ambayo yanaweza kuiimarisha zaidi Chadema kama watatambua walipoanguka na kujirekebisha.
Migogoro katika jamii ni jambo la kawaida, kitu cha msingi ni kwa wanaogombana kurudi mezani na kuzungumza yaishe.
Katika suala hili la Chadema ambalo Zitto Kabwe,
Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wamevuliwa nyadhifa zao na Kamati
kuu ya chama hicho cha upinzania, kila upande bado una nafasi ya
kutafakari upya na kutafuta suluhu kwa lengo la kukijenga chama.
Kwa mfano, kama madai yanayotolewa na kambi ya
Zitto kuhusu matumizi mabaya ya fedha za chama, Mwenyekiti wa chama,
Freeman Mbowe kung’ang’ania madaraka na mengineyo ni ya kweli basi chama
kitumie nafasi hii kujirekebisha.
Vilevile kwa upande mwingine, Zitto na kambi yake watumie nafasi hii kutoa kauli zenye kusuluhisha siyo kujikweza.
Hata kama Zitto ana haki ya kugombea uenyekiti au
cheo chochote, yeye au wanaomuunga mkono hawakupaswa wala hawapaswi
kutoa kejeli kwa uongozi uliopo.
Kauli hizi za kukejeli elimu ya Mwenyekiti wao au
ile kauli ya ‘akili ndogo kuongoza akili kubwa’ ambayo siyo tu imetolewa
kwenye waraka huo bali pia imetumika mara nyingi kwenye mitandao ya
kijamii hazipaswi kuendelezwa kwani zinaudhi na zinaukuza mgogoro.
Zitto na Dk Kitila wajue kwamba, uongozi uliopo
madarakani uko kikatiba. Hata kama wamewazidi elimu au vipaji vya aina
yoyote ile, bado wawaheshimu tu.
Wasubiri muda wa kugombea hivyo vyeo wanavyotaka watamwaga sera zao, lakini siyo kutukana na kukejeli.
Hata hivyo, bado Kamati kuu ya Chadema, ilipaswa
kuwa na subira kabla ya kutoa adhabu kali kama ile. Isitoshe, bado muda
upo, wanaweza kukaa tena na kambi ya Zitto kuzungumza masuala haya kwa
maslahi ya chama. Isitoshe Kamati kuu ya Chadema itoe ushahidi wa
kutosha kwa tuhuma wanazomshushia Zitto kama vile kuchukua posho au
kutumiwa na CCM na idara ya Usalama wa Taifa.
Kimsingi ukisikiliza hoja za pande mbili utaona hiki chama kina
udhaifu mwingi. Tatizo ni kwamba udhaifu huu unazungumzwa hadharani,
badala ya wanaotofautiana kukubaliana na kukosoana.
Hii ni changamoto kubwa katika mfumo wa mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Vyama mbalimbali vimeshindwa kuendelea kwa sababu
ya ubinafsi, majungu na kutokuwajibika. Ni wakati sasa wa pande mbili
hizo kukaa mezani na kusuluhisha tofauti zao, hapo Chadema itaepuka
kikombe hiki cha vurugu.
No comments:
Post a Comment