
Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisisitiza kuwa hesabu za Chadema ni miongoni mwa ambazo hazijakaguliwa, chama hicho kimeishutumu kamati hiyo kwa kuagiza kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa na kusema hatua hiyo ni ubabe.
Wakati Chadema wakitoa kauli hiyo, jana Zitto
alisema vyama vya siasa tisa vikiwamo Chadema, CCM na CUF vinatakiwa
kufika mbele ya PAC Oktoba 25 mwaka huu, kwa ajili ya kujieleza na
kwamba chama kitakachokaidi, sheria za Bunge zinaeleza wazi, kwamba
wahusika wanaweza kufungwa jela siku saba.
Chadema kilisema kuwa PAC kabla ya kuchukua hatua,
ilipaswa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza viongozi wa vyama husika,
kumhoji Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Msajili
wa vyama vya Siasa ambao wameshindwa kutimiza wajibu wa kukagua hesabu
hizo kwa miaka minne.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony
Komu alisema jana kuwa, uamuzi wa PAC utaviathiri vyama kwani bajeti
zake zimezingatia kuwapo kwa ruzuku.
“Kuna vyama ambavyo vinategemea ruzuku kulipa
mishahara ya wafanyakazi wake, Chadema ingawa tuna vyanzo vingine vya
mapato, tunaitegemea kukamilisha bajeti yetu kwa fedha za ruzuku ambazo
zinatusaidia kwa asilimia 45. Ni tabia mbaya kuchukua uamuzi kwa kibabe
na kuhukumu kabla ya kutusikiliza siyo haki hata kidogo,” alisema Komu.
Alitetea chama chake kwamba kimekuwa na utaratibu
wa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa ambapo alitoa ushahidi wa barua ya
Msajili wa Vyama vya Siasa ya April 16, 2012 ikithibitisha kwamba hesabu
zao zipo sawa baada ya kuziwasilisha katika ofisi hiyo.
“Chadema tunataka ukaguzi wa hesabu usijikite
katika fedha za ruzuku pekee bali katika vyanzo vyote vya mapato ya
vyama, tatizo CAG alitueleza kwamba anakabiliwa na upungufu wa
rasilimali watu kwa hiyo PAC walipaswa kuliangalia tatizo hilo na
kutafuta ufumbuzi,” alisema Komu.
Zitto juzi alikaririwa na vyombo vya habari
akieleza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa
vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, lakini vyama hivyo havijawahi
kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake kwa msajili kama sheria
inavyoagiza.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema),
aliamuru Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha utoaji
wa ruzuku hadi hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake
wakuu kuhojiwa.
Miongoni mwa vyama vilivyotajwa ni APPT-Maendeleo
lakini jana Rais Mtendaji wa Chama hicho, Peter Mziray alisema chama
chake hakijawahi kupewa kiasi cha Sh217 milioni kama inavyodaiwa na PAC.
Mziray alikiri walianza kupata ruzuku 2009 ila
inasema ilikuwa kidogo kiasi cha Sh 50,000 kwa mwezi na baadae kupanda
Sh 275,000 kwa mwezi.
Alisema kiasi walichopata kuanzia mwaka 2009 ni
kiasi cha Sh12 milioni tu. “APPT-Maendeleo haina uwakilishi bungeni kwa
hiyo haiwezi kupata kiasi hicho kikubwa cha fedha,” alisema Mziray.
Zitto akaza kamba
Jana Zitto alivitaka Chadema, CUF na CCM kuacha
kupiga kelele katika vyombo vya habari na badala yake viwasilishe
taarifa za ukaguzi wa matumizi yake katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa.
“Vyama hivi visilete ujanja ujanja, hizi ni fedha
za umma lazima zikaguliwe. Tatizo la CCM, CUF na Chadema wanahusisha
suala la kuwasilisha taarifa za ukaguzi na nafasi yangu ya Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema, sifanyi kazi kwa niaba ya Chadema mimi nafuata sheria
za Bunge na katika hili sitacheka na mtu,” alisema Zitto jana wakati
akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo za bunge, Dar es Salaam.
Zitto alisema Kanuni za Bunge zinataka ukaguzi wa
hesabu ya serikali huku akionya kuwa sio sahihi kwa vyama hivyo
kulichukulia suala hilo kama jambo binafsi. Alisema chama husika
kikishakaguliwa na ofisi ya CAG, na taarifa husika hupigwa muhuri wa
ofisi hiyo ya mkaguzi.
Zitto alisema vyama hivyo vinatakiwa kuichukua
taarifa hiyo na kuipeleka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye
hutangaza taarifa hiyo katika gazeti la Serikali ili ijulikane wazi
mapato ya vyama husika.
“Hilo ndio halijafanyika, waulizeni hao CCM, CUF
na Chadema lini wamekaguliwa na kama wamekaguliwa mbona taarifa zao
hazipo katika ofisi ya msajili, sisi tunatambua taarifa za ukaguzi wa
vyama ambazo zipo ofisi ya msajili,” alisema Zitto na kuongeza:
“CCM na Chadema ndiyo wana kelele zaidi, hatuwezi
kusimamia Serikali wakati sisi wenyewe ni wachafu, najua kila mtu
alikuwa akiogopa kueleza ukweli kuhusu ukaguzi kwa vyama vya siasa,
kuanzia CAG, Mwenyekiti aliyepita wa PAC hadi Msajili wa vyama.”
Alisema ruzuku za vyama hivyo ilitakiwa
kusimamishwa tangu miaka mitatu iliyopita, kwa maelezo kuwa Sheria ya
Vyama vya Siasa Ibara ya 14(4) inaeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama
ina uwezo wa kufungia ruzuku ya chama fulani, mpaka hapo
kitakapowasilisha hesabu zake.
“Katika hili CAG na Msajili wa Vyama kila mtu
atabeba mzigo wake, inaonekana kulikuwa na kuogopana lakini mimi
nimekuwa Mwenyekiti wa PAC hivi karibuni lazima nisimamie sheria na hiyo
ndiyo kawaida yangu,” alisema Zitto.
Msajili anena
Msajili wa Vyama vya siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi alizungumza na gazeti dada la The Citizen juzi na kufafanua kuwa
ofisi yake itayafanyia kazi maoni ya PAC na kuongeza kuwa uamuzi wowote
utakaotolewa utafanyika kwa mujibu wa sheria za ofisi yake.
Alisema kuwa alipitia maoni yaliyotolewa na Zitto
kuhusu vyama kufungiwa kupewa ruzuku na kwamba atayafanyia kazi licha ya
kuwa pia alitoa maoni binafsi kuhusu suala hilo.
Alisema hawezi kuchukua hatua za haraka kuchukua hatua za
kuvifungia vyama hivyo mpaka atakapokutana na Makatibu Wakuu wa vyama
hivyo ambavyo vimetajwa na Zitto kwamba havijawasilisha ukaguzi wao.
“Nataka kuzungumza nao ili nijue kwanini wameshindwa kuwasilisha ukaguzi kabla ya kuamua kuchukua hatua za kisheria” alisema.
No comments:
Post a Comment