
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameikataa taarifa ya Serikali jinsi ilivyolishughulikia sakata la ubadhirifu unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji katika Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) visiwani humu.
Msimamo huo wameutoa wakati wakichangia taarifa
iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud Mohamed katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar
kinachoendelea huko Chukwani mjini Unguja.
Mwakilishi wa Mkwajuni Mbarouk Mussa Wadi (CCM)
alisema kwamba Serikali haijachukua hatua yoyote dhidi ya watu
wanaotuhumiwa kuliibia shirika na badala yake imewalinda ikiwemo
kuwahamisha ofisi na wengine kuwapa onyo Meneja Mkuu na wasaidizi wake
Pemba.
Wadi alisema kwamba kitendo kilichofanywa na
Serikali ni sawa na dharau dhidi ya Baraza la Wawakilishi kwa vile
Serikali imeonyeshwa kutotekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya
Fedha ya Baraza la Wawakilishi (PAC) ikiwemo kuchukuliwa hatua za
kisheria watu waliohusika na ubadhirifu huo.
Alisema kamati ya PAC ilipendekeza ufanyike
ukaguzi maalumu ndani ya shirika hilo na kazi hiyo ifanywe na Mkaguzi
Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kupitia mapato na matumizi ya
kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, kazi ambayo haijafanyika kwa zaidi ya
miezi saba tangu kutolewa kwa mapendekezo hayo.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Ali Salum Haji
alisema kwamba kifungu cha 84 cha kanuni za utumishi serikalini
kinaeleza kuwa mfanyakazi anapokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu au wizi
hutakiwa kusimamishwa kazi na kufunguliwa mashtaka na si kuhamishwa
kutoka ofisi moja kwenda nyingine au adhabu ya onyo. Mwakilishi wa
Kiwani, Hija Hassan Hija alisema umefika wakati Baraza la Wawakilishi
lisiunde tena kamati teule za uchunguzi kwa vile Serikali haitaki
kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na Baraza hilo.
Hija alisema tayari kuna ripoti nne za kamati
teule ambazo hazijatekelezwa hadi sasa ikiwemo ile ya uchunguzi wa
uuzaji wa majengo ya umma ya Mambo Msiiige, ubadhirifu unaodaiwa
kufanyika katika Baraza la Manispaa ya Zanzibar, ukodishwaji wa kisiwa
cha Changuu, ubadhirifu wa shirika la Zeco na ununuzi wa mali za
Serikali bila ya kuzingatia sheria ya ununuzi. “Serikali ni dhahiri
inawaogopa watendaji wake au inakusudia kuficha dhambi za wakubwa kuliko
za watendaji, umefika wakati Baraza likatae kuunda kamati za uchunguzi,
hakuna faida kwa wajumbe pia kwa wananchi waliowachagua wawakilishi
wao,” alisema Hija.
Hata hivyo, alisema kwamba huu ni wakati mwafaka
kwa wawakilishi kuwaeleza washirika wa maendeleo wanaochangia fedha za
maendeleo kuwa hazijainufaisha Zanzibar na wananchi wake kutokana na
vitendo vya ufisadi vinavyojitokeza na wahusika kutochukuliwa hatua za
kinidhamu na kisheria.
Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, alisema jukumu la
kikatiba la Baraza la Wawakilishi la kuisimamia Serikali limepotea
kutokana na kuwakingia kifua mafisadi na kusababisha ripoti za Baraza za
uchunguzi kubakia kama boya na wahusika kutochukuliwa hatua za
kisheria.
Salim alisema BLW kuendeleza kuunda kamati za
kuchungua ubadhirifu bila ya wahusika kuchukuliwa hatua kunaendelea
kulishushia hadhi Baraza hilo na kumtaka Spika kutounda tena kamati hizo
kwa vile hutumia fedha za walipakodi bila ya matunda yake kuonekana.
Alisema taarifa ya Serikali ililidanganya Baraza
kutoa mfano katika ripoti ya uchunguzi wa fedha kuwa mtoto wa Rais
mstaafu wa Zanzibar awamu ya sita Shumbana Amani Karume aliundiwa umeme
na kutumika nguzo zaidi ya 40 bila ya malipo, lakini taarifa ya Serikali
imesema ni nguzo 20 kinyume na ukweli ulivyo.
“Ushahidi wa madai hayo upo, hakuna vielelezo
vyovyote vikionyesha malipo alioyafanya, taarifa ya Serikali siiungi
mkono, haina ukweli na hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa
wa ubadhirifu,” alisema Salmin.
Wawakilishi wengine waliopinga taarifa hiyo ya serikali na
kumtaka Waziri Aboud aondoke nayo ni Mwakilishi wa Viti Maalum Asha
Bakari Makame, Mohamed Mbawana Hamad (Chamabani), Ismail Jussa Ladhu
(Mji Mkongwe) Mohamed Haji Rashid, Ali Omar Sheha (Chake Chake) ambapo
Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Makame Mshimba Mabarouk alisema yeye
anaunga mkono taarifa ya Serikali kwa vile ilijadiliwa na kupitishwa na
Baraza la Mawaziri chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein.
Taarifa hiyo imekuja baada ya Kamati ya PAC
kugundua wateja wa Zeco walikuwa wakipewa stakabadhi za malipo kinyume
na malipo halisi, fedha za shirika kuingizwa kwenye akaunti binafsi za
wafanyakazi na wateja wakubwa kuungiwa umeme bure.
Tuhuma nyingine ni pamoja na kampuni binafsi
kuvuta na kufanyakazi za kuunganisha umeme kinyume cha sheria huku mali
za serikali ikiwemo magari kuuzwa kinyume cha sheria ya ununuzi ya umma
pamoja na kuwepo kwa wafanyakazi bandia wa Shirika la Umeme Zanzibar.
No comments:
Post a Comment