
MMILIKI wa Liverpool, John W Henry, alitazama mbali. Utakumbuka tu, wakati alipoingia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuandika kitu kuhusu straika wa timu hiyo, Luis Suarez.
Ilikuwa Julai 24, yaani miezi mitatu iliyopita
ndipo alipotuma maneno yake kwenye mtandao huo. Kilichomsukuma kutuma
maneno hayo ni kitendo cha Arsenal kupeleka ofa ya Pauni 40,000,001
ikimtaka straika huyo raia wa Uruguay.
Dhihaka ya Arsenal ndiyo iliyomfanya mmiliki huyo
wa Kimarekani kuingia kwenye mtandao. Arsenal iliposikia kwamba Suarez
atakuwa tayari kuruhusiwa kuzungumza na klabu yoyote inayomtaka kama
itatolewa ofa inayozidi Pauni 40 milioni, basi yenyewe ikaongeza pauni
moja tu na kuwa 40,000,001 ili wamnase staa huyo.
Hicho ndicho kilichomfanya Henry kwenda kwenye
ukurasa wake wa Twitter na kuwakejeli Arsenal alipoandika: “Hivi ni kitu
gani unafikiria watakuwa wanavuta pale Emirates?”
Juzi Jumamosi, aliingia tena kwenye Twitter na
kuandika tena kitu kinachohusu Suarez. Safari hii aliandika maneno
mawili tu. “Luis. Mchawi.” Ni ngumu kumgomea.
Kwa hali iliyojitokeza kwenye mchezo wao wa juzi
Jumamosi dhidi ya West Brom, hauwezi kumkatalia Henry. Suarez alikuwa
akikimbia uwanjani Anfield akiwa na tabasamu pana, alifunga mabao kama
alivyotaka na kuzima vuruguvugu lote la kutaka kuondoka kwenye usajili
uliopita.
Akafunga ‘Hat-Trick’ yake ya kwanza kwenye Uwanja
wa Anfield, wakati Liverpool iliposhinda mabao 4-1. Suarez angeweza hata
kufunga mabao matano.
Wakati alipokuwa akitoka uwanjani, ikiwa imebaki
dakika moja tu mchezo kumalizika alipofanyiwa mabadiliko, aligeuka pande
zote nne za uwanja na kuwashukuru mashabiki kwa kumpa sapoti.
Mashabiki wa Liverpool hawakuwa wameliondoa penzi
lao kwa straika huyo, lakini kitendo hicho kimezidi kuwarudisha kwenye
himaya yake watu wanaomsapoti.
Kwa maana hiyo, Suarez bado yupo sana Anfield
licha ya Arsenal kumnyemelea, lakini shukrani kubwa kwake Henry, ambaye
hakutaka kabisa kusikia suala kumuuza staa huyo.
Labda angekubali kumuuza kama kungekuja ofa ya nguvu na angefanya hivyo kwa klabu inayotoka nje ya England.
Henry alifahamu wazi kumuuza Suarez ni kuishushia
hadhi Liverpool na hakutaka klabu yake ionekane dhaifu kwa kushindwa
kugomea klabu nyingine zinapojaribu kuwavamia na kutaka mchezaji kwao.
Kwenye Uwanja wa Anfield juzi Jumamosi, Suarez alionyesha kwa
nini Henry alipambana kuhakikisha anabaki. Staa huyo tangu alipoingia
uwanjani kupasha misuli akiwa na straika Daniel Sturridge, alionyesha
wazi kwamba kuna kitu anataka kukifanya kwa ajili ya mashabiki wake.
Kabla hata hajatumbukiza mipira wavuni, alikuwa
akiwakimbiza na kuwasumbua mabeki wa West Brom muda wote na hivyo
kumchoka kumzuia. Suarez alicheza kwenye ubora wake.
Imani ya Liverpool imezaa matunda, kwa sababu
pamoja na Suarez kuwatikisa kwenye kipindi cha usajili akitaka kuondoka,
uamuzi wao wa kumbakiza haukuwa na shaka kwamba angecheza chini ya
kiwango kwa sababu wanafahamu hilo si asili yake.
Wanaokwenda kumtazama mazoezini, wale wanaokuwa
karibu naye kwenye kikosi, wanamfahamu staa huyo alivyo na moyo wa
kupambana muda wote na kiu yake ni kufikia mambo makubwa kwenye soka.
Mazoezi anayoyafanya kama ni mchezaji kinda anayetafuta namna ya kutaka
kutambulika.
Dhidi ya West Brom alikuwa anafunga huku
akitabasamu na hilo linadhihirisha kwamba anachokifanya kinatoka moyoni
na anacheza mpira kwa mapenzi yake.
Kwa mujibu wa Suarez sababu moja inayotaka
kumwondoa Liverpool ni kushindwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini
kwa kiwango cha timu hiyo kwa msimu huu imani ni kubwa kwamba msimu ujao
wanaweza kuwamo kwenye michuano hiyo. Ni jambo la kusubiri.
Ni jambo linaloeleweka, wachezaji wote makini
wanahitaji kucheza kwenye michuano yenye hadhi kubwa. Kocha Brendan
Rodgers anaonekana kuzichanga vyema karata zake na msimu ujao Liverpool
inaweza kuzungumziwa kwenye mikikimikiki ya Ulaya.
Lakini, kabla ya kulifikia hilo, shukrani kubwa ni
kwa Henry aliyepambana kumbakiza Suarez Anfield na sasa mchezaji huyo
anatema cheche.
No comments:
Post a Comment