
Afya za Watanzania zipo hatarini kutokana na kula unga ulioandaliwa bila kuzingatia kanuni za afya na kwenye maeneo machafu.
Unga huo ambao umesambaa madukani huandaliwa kwenye mashine ndogo za kusaga, zilizopo katika mitaa ya miji mikubwa nchini.
Bidhaa nyingine za nafaka ambazo zinauzwa na
wafanyabiashara hao mitaani bila ya kufuata kanuni za afya ni unga wa
ngano, ulezi, mtama, muhogo na uwele.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa
wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakianzisha miradi ya kusaga mahindi na
unga wake kuwekwa katika vifungashio, bila ya kufuata taratibu za afya
zilizowekwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango
Tanzania (TBS).
Kwa mujibu wa ripoti ya miaka 10 ya utendaji kazi
wa TFDA, kifungu namba 28 cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura
ya 219, inazuia mtu yeyote kuzalisha, kuingiza, kusambaza na kuuza
nchini chakula kilichofungashwa kabla ya kusajiliwa na mamlaka.
TFDA katika ripoti hiyo ilifafanua kuwa vyakula
ambavyo havijafungwa kama matunda na nafaka hukaguliwa kwa kuchukuliwa
sampuli, ambazo hufanyiwa uchunguzi wa kimaabara na uchanganuzi wa
madhara yanayoweza kutokea.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwa
katika mitaa mingi ya Jiji la Dar es Salaam, wafanyabiashara hao husaga
unga wa mahindi na kuuweka katika vifungashio vya kilo tano, 10, na 25.
Msemaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
Roida Andusamile, alisema jukumu lao ni kusimamia bidhaa zilizopo sokoni
kwa kukagua ubora wake, lakini wanapata wakati mgumu kwa
wafanyabiashara ambao wapo vichochoroni na wanakwepa kufuata utaratibu
kwa makusudi.
Aliongeza kuwa kila bidhaa ambayo wameikagua ina
nembo ya ubora au mhuri wao, kitu ambacho ni rahisi hata kwa walaji au
watumiaji kutoa taarifa pindi wanapoona bidhaa haina mhuri huo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, wasagaji
wa unga wamekuwa hawafuatia sheria inayowakataza kuzalisha bidhaa zao
kwenye mazingira machafu.
Mtaalamu wa chakula wa TFDA, Kyaruzi Jason alisema
kuwa bado wana kazi kuwafikia wananchi hasa wasindikaji wadogo kutokana
na kukosekana kwa ushirikishwaji wa sekta nyingine.
Alisema hakuna mpangilio maalumu wa maeneo ya
viwanda, hali inayowafanya washindwe kuwafikia wasindikaji wote, hasa
walio maeneo ya vichochoroni.
Madhara ya unga huo
Uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya unga huo
umeanza kuleta madhara kwa watumiaji, ikiwemo kusababisha ugonjwa wa
kuhara. Wengine hushindwa kuutumia kwa sababu una ladha chungu, wenye
rangi nyeusi kwa mbali na harufu mbaya.
“Usinunue kwenye duka la hapo kona nunua katika
duka la mbele hilo unga wake ni mchungu na mweusi,” alisikika mama mmoja
akimuonya mwanaye.
Gazeti hili lilifanya uchunguzi katika baadhi ya
mashine za kusaga za Jiji la Dar es Salaam hasa maeneo ya Mbagala,
Manzese na Tandale na kushuhudia mahindi yakiingizwa katika mashine ya
kusaga bila ya kuondolewa uchafu.
Uchunguzi ulibaini baadhi ya mashine hizo zipo
katika mazingira ya uchafu, ikiwemo mifereji ya maji machafu kupita
karibu na mashine hizo, pia maeneo yalipo mahindi hayo kuhifadhiwa
bidhaa nyingine kama mafuta ya taa, dawa za kuulia wadudu, sabuni na
bia.
Mbali ya kuhifadhiwa katika mazingira mabaya
mwandishi wa habari hii alishuhudia baadhi ya wasindikaji wakisaga
mahindi hayo bila ya kuangalia kama kuna mawe, mabaki ya magunzi wala
takataka nyingine.
Godfrey Kibatwe, mkazi wa Mbagala jijini Dar es
Salaam ambaye ni mmoja wa vijana wanaofanya kazi kwenye moja ya mashine
za kusaga nafaka zilizopo katika eneo hilo, alisema wao kazi yao siyo
kusafisha mahindi bali ni kusaga na kuweka kwenye vifungashio kulingana
na makubaliano yao na mwenye mashine.
Alisema kazi ya kuondoa uchafu katika mahindi
yanayosubiri kuingia kwenye mashine ni kubwa, hivyo inahitaji vibarua
ambao wanalipwa na mwenye mahindi.
Kibatwe alisema wanachofanya wao ni mahindi hayo
au nafaka nyingine kuipitisha kwenye chekeche kutoa vumbi na kama kuna
uchafu mwingine huwa hawauangalii.
Omari Mtagwa ni kijana ambaye hufanya kazi za
kusaga unga maeneo ya Mabibo jijini Dar es Salaam, alisema kuwa wao
husaga kulingana na makubaliano na tajiri ambapo tani moja husaga kwa
kiasi cha Sh30,000 au 40,000 kulingana na uwezo wa tajiri lakini haiwi
chini ya hapo.
Alisema bei hiyo ni tofauti na kusaga na kukoboa
ambapo kukoboa ni Sh20,000 kwa tani moja ambayo ni sawa na kilo 1,000,
kazi ambayo huifanya kwa siku nzima.
Kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Prosper
anauza duka maeneo ya Tandika, ambapo dukani kwake kuna unga wa aina
tatu na bei tatu tofauti. Upo wa Sh1,400, 1,300 na 1,100, namuuliza
sababu za kuwepo aina hizo tatu za unga anasema kuwa ni kutokana na
kutofautiana ubora ambapo huo wa bei kubwa ni mweupe hata ukiutizama
tofauti na wa Sh1,100.
“Hata tunaponunua kwa wauzaji wa jumla kuna wa bei nafuu na wa
bei kubwa kulingana na ubora wake kwa macho na kwa kuukamata mkononi,
kwa kuwa tumeuza siku nyingi tunajua, na ndiyo maana hata sisi tunauza
bei tofauti,” alisema Prosper.
Kijana mwingine anayefanya kazi hiyo Tandika Kwa
Maguruwe jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Bob,
alisema kuwa kazi hiyo ni ngumu na inahitaji nguvu sasa kama watafanya
na kazi ya kuchambua uchafu kutoka katika mahindi hayo itachukua muda
mrefu kuimaliza.
“Kazi hii inatofautiana kulingana na tajiri,
wengine wapo makini na wanaweka watu wa kuyamwagia maji kabisa, lakini
wengine hawana huo mpango na sisi tunafanya kulingana na wao
wanavyotulipa, wakitulipa vizuri na kuwa makini kama hao wengine kwa
nini tufanye kazi mbaya,” alisema.
Bob alikiri kuwa hata yeye amewahi kula unga ambao
ulikuwa na wadudu, lakini kwa kuwa anajua tatizo lipo wapi hakuwa na
sababu ya kumlaumu mwenye duka zaidi ya kuwaambia wana familia wake
wahame na kununua katika duka lingine.
Alisema utofauti wa ubora wa unga unatokana na
mahindi anayoleta tajiri yaani anayetaka kusagiwa na maelekezo yake,
kuna ambaye anataka yapitishwe kwenye mashine kama ada badala ya
kukobolewa sana na kuna anayeagiza yakobolewe sana na kuajiri wapetaji
ambao hupeta kwa usimamizi maalumu.
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kkuu cha Mzumbe
Morogoro, alisema kuwa sheria nyingi zilizopo hazifanyiwi kazi kutokana
na kuingiliwa na wanasiasa.
“TBS wana dhamira na sheria zao lakini tatizo ni
utekelezaji wake kutokana na miundombinu, lakini vile vile sheria nyingi
zinaingiliwa na wanasiasa kwa mfano kuna maeneo hao wasindikaji wadogo
wamewekwa na viongozi ambao wanahitaji kupata kura kutoka kwao, hivyo
inakuwa ngumu utekelezaji kwani hawa wanaweza kusema hivi wale wakasema
vile,” alisema Profesa Shumbusho.
Dk Raymond Mwenekano wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, anayataja madhara ya ulaji wa vyakula vilivyoandaliwa bila
uangalizi maalumu kuwa ni kupata magonjwa kama vile kansa ya utumbo,
mwili kuwasha, kubabuka na vidonda mwilini.
“Madhara yake ni makubwa, ndiyo maana siku zote
tunasisitiza kula vyakula vilivyoandaliwa kwa umakini na uangalizi
maalumu ili kuepuka madhara kama hayo ambayo mara chache huwa ya muda
mfupi lakini mara nyingi huwa ni ya muda mrefu na ni vigumu mtumiaji
kujua kuwa hayo madhara aliyapata kwa kula vyakula hivyo,” alisema
Mwenekano.
No comments:
Post a Comment