
KAMA siku muhimu zaidi katika historia ya taifa la Zimbabwe, Alhamisi ya tarehe 17 Aprili 1980, wananchi wa Zimbabwe kwa uwingi wao wanakutana katika uwanja wa taifa mjini Harare. Baada ya uhuru wa wachache panapo mwaka 1965, harakati za kuikomboa Zimbabwe zikaendelea kupamba moto hadi siku hiyo ambapo walowezi wanainyoosha mikono yao juu na kukubali kuiachia nchi nzuri kama Zimbabwe.Ni siku ambayo nchi yao inapata uhuru kutoka kwa wanyonyaji na wakoloni akina Ian Smith. Kwa mwananchi yeyote ambaye amekishuhudia kipindi cha nchi kukaliwa na wakoloni, ni siku ambayo kamwe haiwezi kufutika katika kumbukumbu yake.
Viongozi wa mataifa mbalimbali ya Kiafrika wakahudhuria sherehe hizo. Lakini pamoja nao, mwanamuziki maarufu wa miondoko ya Reggae, Robert Nesta Marley almaarufu Bob Marley anaalikwa rasmi kutumbuiza katika sherehe hizo. Bila shaka haikuwa imetokea kwa bahati mbaya kwa waandaaji wa sherehe hizo kuamua kumwalika mwanamuziki huyo aliyevuka bahari kubwa ya Atlantiki kutoka nchini mwake Jamaika huko Karibiani hadi kusini mwa bara la Afrika.
Nasema haikuwa bahati mbaya kumwalika, kwani kibao chake mahsusi kwa nchi hiyo kilichobatizwa jina la “Zimbabwe” kilishiba ujumbe maalumu kwa nchi hiyo. Na tangia kipindi hicho, ama pengine hata kabla ya kipindi hicho, kiongozi wa Zimbabwe Bw. Robert Gabriel Mugabe ameondokea kuwa mshabiki mkubwa wa Bob Marley. Na kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Mugabe hutoa kiasi fulani cha pesa kila mwaka kwa taasisi ya hayati Bob Marley aliyeaga dunia takribani mwaka moja baada ya Zimbabwe kupata uhuru.
Siku hiyo ya uhuru wa Zimbabwe, mbele ya marais kadhaa wa nchi za Kiafrika na wageni wengine kutoka kwingine duniani, Bob Marley hakusita kutoa nasaha zake kwa nchi hiyo kupitia kibao chake cha Zimbabwe. Sitaki kuamini kwamba baada ya takribani miaka 27 tu, kuna uwezekano wa Bw. Mugabe kuwa amekisahau kabisa kile ambacho rafiki yake amekuwa akikiamini na kukihubiri hadi pale mauti yalipomfika.
Katika kuanza ubeti wa kwanza, Bob Marley aliwaambia Wazimbabwe na walimwengu wengine kote na hususani wale wakandamizaji. Aliwaambia kwamba, kila mtu anayo haki ya kujiamulia mustakabali wake alimradi katika hayo maamuzi yake asivunje sheria. Na kwamba wao (Wazimbabwe) kwa umoja wao, bega kwa bega wamepambana mapambano ambayo ndiyo iliyokuwa njia ya pekee kwao kuyatatua matatizo ya kunyonywa na kukandamizwa.
Masikini ya Mungu, mwanamapinduzi Bob Marley akaenda mbali katika ubeti wa pili na kuwaasa zaidi Wazimbabwe kwamba, hakuna haja ya kugombania madaraka katika Zimbabwe huru. Na mbali zaidi, kama nabii, na pengine ni kweli alikuwa nabii. Maana sasa tumeanza kuona maana ya kile ambacho Bob Marley alikihubiri. Aliwahakikishia Wazimbabwe na hata Waafrika wengine kwamba muda si mrefu tungemfahamu nani ndiye mwanamapinduzi halisi. Na hakuwa ametaka watu wake (watu weusi na Waafrika wengine) walaghaiwe.
Na katika kumalizia kibao hicho mahsusi, Bob Marley akasema kwamba kugawa na kutawala (to divide and rule) kama ilivyokuwa sera ya wakoloni kusingewafaa wao kwani kungewasambaratisha. Akazidi kusisitiza juu ya kwamba si punde tungewafahamu wale wanamapinduzi wa kweli. Imani yake ilimtuma kuamini ya kuwa hata katikati ya watu weusi wa Afrika bado wote si ndugu wenye dhamira moja.
Baada ya kuzipitia nasaha za Robert Marley kwenda kwa wananchi wa taifa linaloongozwa na Robert Mugabe, nakuja kuelewa kwamba RM pengine alikuwa ameupoteza tu muda wake kumpa ujumbe mtu kama RM. Sote tunafahamu nini kinatokea Zimbabwe baada ya mwaka 2000 pale Mugabe alipowanyang’anya ardhi wakulima wa kizungu. Labda hilo si tatizo sana kwa watu duni wa Zimbabwe. Kama madhara ya kuanguka kwa uchumi wa nchi yanamgusa kila mtu nchini humo basi nashawika kuamini kwamba hilo ni tatizo kubwa zaidi kwa mtu wa hali ya chini zaidi.
Kiburi cha Bw. Mugabe hakikomei pale, kinaendelea hadi pale anapofikia kuzikandamiza haki za raia. Harakati za kisiasa katika upinzani zimekuwa jehanamu kwa wanaharakati hao. Sijui ni nini ambacho Mugabe anakiamini katika falsafa ya rafiki yake Bob Marley. Kama rafiki yake huyo alitanabaisha kwamba kila mtu anayo haki yake ali mradi asivunje sheria, inakuwaje yeye hajisikii kabisa kuitoa haki hiyo kwa wananchi wake?
Ni nini itakuwa tiba sahihi ya kansa hii miongoni mwa viongozi wengi wa Kiafrika wanaolazimisha kwamba upinzani ni uhaini? Mugabe hataki kabisa kukiachia kiti cha urais katika Zimbabwe. Hapa sasa ndipo anapopingana na ubeti wa pili katika nasaha kutoka kwa rafikiye Bob Marley. Falsafa ya Bob Marley ilikuwa, hakuna haja ya kugombania (kung’ang’ania ndiyo ingekuwa lugha nzuri zaidi) madaraka katika Zimbabwe huru. Nina hakika sasa kwamba mwanamuziki huyo mwanamapinduzi alifahamu nini kingeweza kutokea mbele ya safari.
Kuna haja gani ya kung’ang’ania madaraka katika umri wake wa miaka 85? Ukweli hapa unajidhihirisha wazi kuwa Mugabe anakiogopa kivuli chake na angependa kufia madarakani ili kutokumbwa na ‘jini’ kama lililowakumba Kenneth Kaunda na Frederick Chiluba, jirani zao. Jini ambalo bado linamwandama Big Ben ‘Mr. Clean’. Malipo ya kila uovu yapo mumu humu duniani. Lakini anasahau, unaweza kuwapumbaza watu fulani kwa wakati fulani, lakini kamwe hutoweza kuwapumbaza watu wote wakati wote.
Muda wake sasa umefika mwisho, huo ni ukweli, hawezi kamwe kushindana na muda. Hata ile heshima ya kuwa mpigania uhuru sasa hanayo tena kwani yale ambayo watu weusi tulipigana kuyaondoa barani mwetu, ndiyo anayaoyatekeleza kwa sasa. Sauti za wanyonge zinanyamazishwa kinguvu. Unaona kilichompata Morgan Tsvangirai na wafuasi wake? Viongozi wengi wakiongozwa na Mugabe wanatulazimisha tuamini kuwa viongozi wa vyama vya upinzani ni wavunja amani, ni wahaini na wasiojua maana ya demokrasia. Lakini viongozi wa upinzani hawana jeshi wala polisi wala silaha kali za kivita. Inashangaza pale harakati zao zinaponyamazishwa kwa nguvu kubwa.
Wengine wanasema Morgan ni kibaraka wa mabepari wa Magharibi. Inawezekana ikawa hivyo kwa sababu hata mazingira yanashawishi hivyo. Lakini wakati fulani tuketi chini na kutafakari falsafa ya mwanareggae mwingine Lucky Dube pale alipouliza, "do you wanna be a well fed slave, or the hungry free man?" Kipi ni muhimu zaidi kwa Wazimbabwe kwa sasa? Ni kuwa huru chini ya maisha magumu kupindukia na kipindupindu kilichokithiri ambacho kimewatumbukiza katika shimo lisilo na kina, ama kwa mwamvuli mwingine na ahueni ya maisha? Pengine uzalendo tafsiri yake sahihi ni kuteseka na kufa na tai shingoni.
Na viongozi wa Afrika wamekuwa wakimpa sana kiburi Mugabe. Tunashukuru sasa nao wameshituka hata wanamtaka aheshimu haki za raia. Nadhani Waafrika tumechoka sasa kutokuwa huru hata ndani ya Afrika huru. Mugabe anapaswa kufahamu, Zimbabwe siyo mali yake peke yake, ni mali ya binadamu wote wanaoheshimu kanuni na sheria. Wanaoheshimu haki na utu wa watu wengine. Wanaojua kupingana pasipo kupigana. Hiyo ndiyo demokrasia tunayopaswa kuihubiri hata mataifa mengine yanayojionea namna tunavyoshindwa kujitawala yatupe heshima.
Kwa kuwa naambiwa Mugabe ni mshabiki mkubwa wa Bob Marley, ningependa kumkumbusha kuwa rafiki yake huyo alikuwa ni muumini mzuri wa haki za raia na usawa miongoni mwa watu wote, duniani kote. Na kama amesahau kidogo, labda kutokana na umri wake kuwa mkubwa, ama ametingwa sana na kuwaadabisha wapinzani hata akakosa muda wa kuusikiliza kwa tuo muziki wa kipenzi chake, kuwa mwanamuziki huyo pia alitengeneza kibao kilichozungumzia vita barani Afrika, akakiita War, kwa maana ya vita.
Namkumbusha kuwa, katika ubeti wa pili na wa mwisho katika kibao hicho ndimo kuna ujumbe mahsusi kwake na kwa viongozi wengine wa sampuli yake. Kwa hisia za kweli, zenye kuchoma, Bob Marley anasema, “Bara la Afrika halitojua amani, sisi Waafrika tutapigana ikibidi, na twajua tutashinda kwani twaamini wema hushinda uovu…..”
Wazimbabwe sasa watalazimika kutumia nguvu kumng’oa Mugabe. Askofu wa Kikatoliki, Pius Ncube aliwaamsha Wazimbabwe, waandamane kwa nguvu zote hadi waweze kumwondoa madarakani. Askofu Ncube alisema yupo tayari kutazamana na mitutu ya bunduki hata kama itauondoa uhai wake. Mwanamapinduzi, Askofu Pius Ncube alijiamini kusema hivyo kwani anayo imani kuwa siku zote wema hushinda uovu kama ilivyo falsafa ya hayati Robert Nesta Marley, mwanamuziki kipenzi cha mtawala Robert Gabriel Mugabe. Wote wanaitwa Robert lakini wenye kutofautiana kabisa falsafa zao. Askofu Pius Ncube akafikia hatua ya kutengenezewa kashfa na wanausalama ili kumfunga mdomo. Na juzi tu, Vatican City wamempiga marufuku kuzungumzia tena masuala ya siasa. Yeye anasema pamoja na kushushwa cheo hadi kubakia daraja la kawaida la Upadre, bado ataendelea kuiombea Zimbwabwe na raia wote wa Zimbwabwe wanaoteseka.
Wazimbabwe watashinda tu, na wengine wote wanaokandamizwa Afrika nzima, kwani siku zote wema hushinda uovu.
No comments:
Post a Comment