
KATIKA fukwe za Kitongoji cha Funchal visiwani Madeira, mwishoni mwa miaka ya 1980, mtoto mmoja maskini shombeshombe wa Kireno alikuwa akikimbiza kaa kwa ajili ya kuwauza kwa watalii waliokuwa wanazurura katika visiwa hivyo.
Baba wa mtoto huyu alikuwa mlevi mkata majani wa
manispaa, mama yake alikuwa mpishi asiyevutia kwa sura wala umbile,
nyumba yao ilikuwa duni na hafifu kiasi kwamba wanaume na wanawake
waliishi katika chumba kimoja.
Sasa mtoto huyo ndiye Cristiano Ronaldo
unayemfahamu. Huyu huyu ambaye unamwangalia kwa jicho la husuda akiwa
amevaa miwani yake ya jua aina ya Prada, viatu vyenye thamani ya nyumba
moja Temeke, raba za kisasa zilizotengenezwa kwa ajili yake na nguo za
wabunifu kutoka Kampuni ya Armani nchini Italia.
Maisha ndivyo yalivyo. Alikopitia kufika alipo
inabakia kuwa historia ambayo kila mtu anaifahamu. Lakini anaporudi tena
katika fukwe zile zile za Funchal alizokuwa anakimbiza kaa kwenda
kuwauzia watalii, huwa analala katika boti yake ya kifahari na mrembo
wake Irina Shayk huku watalii wale wale wakimshangaa kwa jicho la
husuda.
Siku chache zilizopita, Ronaldo amesaini mkataba
mpya wa kuichezea Real Madrid. Mkataba ambao unamwacha akiwa mwanasoka
anayelipwa zaidi duniani kuliko wote. Euro 17 milioni kwa mwaka baada ya
makato ya kodi. Kwa sasa ana umri wa miaka 28. Alizaliwa Februari 5,
1985 siku ile ambayo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinatimiza miaka
minane tangu kianzishwe. Mkataba wa sasa utamfanya apokee kiasi cha
Euro 17 milioni kwa mwaka mpaka atimize miaka 33 mnamo Juni 2018 wakati
huo timu zikianza kuwasili viwanja vya ndege Russia kucheza Kombe la
Dunia.
Mkataba wake ameupata kwa kuutumia mgongo wa
Manchester United. Amewatumia bila ya wenyewe kujijua. Shukrani kwa kazi
nzuri ya watu wake wa masoko na matangazo ambao wamemzunguka.
Picha aliyoicheza kwa msimu mzima ni kwamba
alikuwa hana uhakika na maisha yake Santiago Bernabeu. Alianza msimu
uliopita katika pambano dhidi ya Granada ambapo alifunga mabao mawili na
akagoma kushangilia kwa madai hana furaha.
Wengi wakaanza kubashiri kwamba Ronaldo alikuwa
njiani kurudi Manchester United. Msimu huu wakati dirisha la uhamisho
likikaribia kufunguliwa, watu wake wanaomzunguka wakafanya kazi nzuri ya
kueneza uvumi kwamba kulikuwa na uwezekano wa yeye kurudi Old Trafford.
Lengo lake pamoja na wakala wake, Jorge Mendes,
lilikuwa ni kuishtua Real Madrid kumpatia mkataba mwingine haraka sana.
binafsi nilikuwa sioni uwezekano wa Ronaldo kucheza kwingine kokote
zaidi ya Real Madrid.
Kwa sasa amesimama juu ya Manchester United.
Wamarekani kina Glazier hawawezi kumlipa Pauni 300,000 kwa wiki baada ya
kodi. Kwenda PSG na Man City nalo ni jambo gumu kwa sababu ni timu
ambazo zingepunguza heshima ya jina lake hasa wakati huu ambao
anapambana na Lionel Messi katika Ufalme wa soka duniani.
Isingewezekana fahari wako akacheza Uwanja wa Nou
Camp kila wikiendi wakati wewe unacheza Etihad au Parc des Princes
katika timu ambazo hazina historia nene kama Barcelona, Man United, Real
Madrid au AC Milan. Ni lazima ufalme wake ungeshuka ghafla. Wakati
mwingine pesa si kila kitu maishani.
Timu pekee yenye uwezo wa kumpa Ronaldo kila kitu
maishani kwa sasa ni Real Madrid. Inaweza kumpa Euro 17 milioni kwa
mwaka, inaweza kumpa mataji, inaweza kumpa matangazo ya biashara na
zaidi ya yote inaweza kumletea mashabiki 85, 454 kila mwisho wa wiki
huku akiwa amevaa jezi aliyokuwa akivaa Raul Gonzalez Blanco.
Kurudi Manchester United ndiyo uwezekano pekee ambao ulikuwa
unamtisha Fiorentino Perez. Ndiyo silaha pekee ambayo Ronaldo na watu
wanaomzunguka walikuwa wanaitumia katika kumtisha Perez. Alikuwa akisaka
pesa na ngao yake ya kujikinga ilikuwa Old Trafford.
Kikubwa zaidi Ronaldo na maringo yake ya ujana
alihitaji pesa za kuingiza jina lake katika historia kama Mwanasoka
anayelipwa zaidi duniani. Anataka achezee pesa, aogelee katika pesa,
azilalie pesa. Asahau kila kitu kilichotokea katika maisha yake Funchal
akiwa anakimbizana na Kaa kwa ajili ya kuwauza kwa watalii.
Anataka kuishi katika dunia anayoishi Floyd
Mayweather, David Beckham, Puff Daddy, Thom Cruise na wengineo. Huu bila
shaka ndiyo mkataba wake wa mwisho mnono katika maisha yake ya soka.
Juni 2018 wakati timu zikiwasili Russia katika
Kombe la Dunia, Ronaldo atakuwa amekaribia kusaini mkataba na Sporting
Lisbon, Benfica au Porto hili akazifahidi pesa zake vizuri katika ardhi
ya kwao Ureno. Mpira utakuwa umeondoka kwa kiasi kikubwa mguuni.
No comments:
Post a Comment