Blogger Widgets

Friday, 18 October 2013

Nguvu ya CCM ipo ndani ya Kinana?


Historia na utendaji wa vyama vya siasa nchini inaonyesha kuwa mara baada ya kuanzishwa, vyama vya upinzani, kwa ujumla wake vilikuwa dhaifu. Ni kweli kulikuwa na NCCR-Mageuzi ambayo iligeuka kuwa tishio kiasi kwamba baadhi ya watu wakadhani ndiyo ingeweza kukimaliza Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, baada ya muda, NCCR-Mageuzi ikafifia na kuiacha CCM ikiendelea kutamalaki.
Baadaye kikaibuka Chama cha Wananchi (CUF) na kuichachafya CCM hadi baadhi ya watu wakaamini kuwa ndiyo ule ukombozi wa kweli wa Mtanzania kutoka chama hicho tawala ambacho kimekuwa madarakani tangu kupatikana kwa uhuru. Nayo ikafifia na kuiacha CCM ikiendelea kutawala.
Labda hicho kilikuwa kipindi cha mpito. Kilikuwa ni kipindi cha vyama kujifunza jinsi ya kuendesha siasa za vyama vingi. Kumbuka kuwa kabla ya hapo waliokuwa wanaendesha vyama vya upinzani walikuwa hawana uzoefu wa kuwa wapinzani. Hivyo, walikosa maarifa ya kukabiliana na siasa, mikakati, propaganda na sera za chama tawala.
Baadaye kikaubuka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kikaja kwa kasi sana kiasi kuwa wakati fulani ilifikia hatua badala ya wapinzani kuwa wanajibu mapigo ya CCM, chama hicho tawala ndicho kikageuka kuwa ndicho kinajibu kutoka kwa Chadema.
Bado Chadema inaendelea na kazi hiyo kama tunavyoshuhudia hivi sasa kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya ambapo kwa mara ya pili Rais Jakaya Kikwete amelazimika kukutana nao ili kuweka sawa baadhi ya mambo katika mchakato huo.
Ukiangalia kwa makini kuibuka kwa Chadema na nguvu hizo utabaini kuwa si nguvu zake pekee, kwa kiasi kikubwa, udhaifu wa CCM yenyewe umechangia kukidhoofisha na kuifanya Chadema iibuke kwa nguvu.
Kuna sababu kadhaa zilizokidhoofisha CCM na nyingi ya sababu hizo ni za ndani. Inaelekea ilifika wakati chama hicho kikajisahau, hasa baada ya wapinzani kuibuka na kuzama na kudhani kuwa hakuna mpinzani ambaye anaweza kukiletea madhara.
Hali hii ikakifanya chama hicho na viongozi wake kubweteka. Ikatoa nafasi kwa Chadema, ambayo ilikuwa imeshajifunza kupitia makosa ambayo yalifanywa na watangulizi wake, kuishika CCM barabara.
Lakini pia kulikuwa na migogoro ndani ya CCM iliyozalishwa na vita vya madaraka. Wengi wanadhani kuwa migogoro hii imeanza siku za karibuni lakini ukichunguza kwa undani utabaini kuwa asili ya migogoro hii ni tangu kuteuliwa kwa Benjamin Mkapa kuwa mgombea wa chama hicho mwaka 1995. Wakati huo, ambapo ilikuwa imepita miaka 10 tangu Mwalimu Julius Nyerere kung’atuka kwenye uongozi, wengi walishaweka tamaa ya kuchukua nafasi hiyo.
Hata hivyo, hawakujua kuwa bado Nyerere alikuwa na uwezo mkubwa wa kuathiri uamuzi ndani ya chama. Kilichotokea wakati wa uteuzi mwaka 1995 kiliwafanya waanzishe harakati na mikakati ya chini kwa chini ndani ya chama ili kuhakikisha kuwa inapofika wakati wa uteuzi mwingine hawapigwi chini. Ndiyo njia ambayo ilitumiwa na Rais Kikwete.
Kwa muda mrefu, tangu Rais Kikwete kuingia madarakani, hata uongozi ndani ya chama ulishindwa kutulia na kufanya kazi ya siasa kutokana na migogoro hii. Hivi sasa hali inaelekea kutengemaa baada ya kuteuliwa kwa Abdulrahman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Hata watumishi wengine ndani ya chama wanakiri kuwa kuteuliwa kwa Kinana kumehuisha chama hicho kwa sababu hivi sasa kazi si tu zinafanyika, bali zinaonekana kufanyika. Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao wanabainisha kuwa kama si umahiri wa Kinana, hivi sasa Chadema kingekuwa imekifikisha CCM mahali pabaya.
 “Kuna wakati kazi za chama zilikuwa zinafanywa kwa kuzingatia nadharia za kwenye vitabu kuliko hali halisi. Matokeo yake chama kikaanza kupoteza mvuto kwa watu wa kawaida. Lakini tunashukuru hivi sasa kuwa CCM kimerejea kwenye nafasi yake kama chama cha kutetea wanyonge,” anabainisha mfanyakazi mmoja kutoka Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
Tangu kuteuliwa kwake miezi kadhaa iliyopita, Kinana tayari ameshafanya ziara katika zaidi ya nusu ya mikoa yote Tanzania Bara. Ziara hizo zimemwezesha kuona kwa uhalisia matatizo yanayokikabili chama hicho na hivyo kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutafuta ufumbuzi wake.
 “Unapozunguka huku vijijini unapata nafasi ya kujionea na kusikia moja kwa moja kutoka kwa wanachama kuhusu matatizo wanayokabiliana nayo… kama ukikaa ofisini tu na kusubiri ripoti za watendaji kila siku utakuwa unaongopewa tu,” anasema Kinana.
Katika mahojiano hayo, Kinana anasisitiza kuwa uhai wa chama kwa kiasi kikubwa unategemea wananchama. Anasema kuna makosa yanafanyika ndani ya chama kwa viongozi kudhani kuwa chama ni ngazi za uongozi.
“Wasichokifahamu viongozi wengi ni kuwa katika ngazi za juu za chama hakuna wanachama… hakuna wanachama kwenye halmashauri kuu ya taifa, hakuna wanachama kwenye ngazi ya mkoa na wilaya. Wanachama wapo kwenye shina. Huko ndiko ambako tunapaswa kukutilia mkazo,” anasema.
Anawataka viongozi wa mikoa na wilaya wasikae tu ofisini na kusubiri ripoti kutoka ngazi ya chini. Wanapaswa kutoka ofisini na kutembelea mashina ambako watakutana na wanachama.
Katika ziara yake ya karibuni iliyomchukua siku 18, akiambatana na Katibu wa Uenezi na itikadi, Nape Nnauye, Kinana amekuwa akiwakemea viongozi wa Serikali ambao wamekuwa na tabia ya umangimeza na uzembe wa kushughulikia matatizo ya wananchi.
Kimsingi, Kinana anabainisha kuwa kuna viongozi wa serikali ambao wanaonekana kuwa wamesahau kuwa wanapaswa kutekeleza sera za CCM ambayo ndiyo iliyoiunda Serikali wanayoitumikia.
Kinana alitumia ziara hiyo kuwaonya watendaji hao wabovu na kuwataka kuacha tabia ya umangimeza. Alisema CCM kimekuwa kikilaumiwa kutokana na kukwama kwa miradi mingi ya maendeleo lakini ukichunguza kwa umakini utabaini kuwa katika maeneo mengi kukwama huko hakutokani na mipango mibaya, bali uzembe wa watendaji wa serikali kutekeleza mipango iliyopo kwa ufanisi.
Mathalan, akiwa katika kijiji kimoja katika jimbo la Solwa mkoani Shinyanga, msafara wake ulisimamishwa na wanakijiji waliokuwa wanalalamika kwa nini hawapati maji safi wakati bomba kubwa la maji kutoka Ziwa Victoria linapita hapo.
Alipowauliza viongozi wa mkoa waliokuwa wameandamana nao, Kinana aliambiwa kuwa kuna mradi mwingine wa kusambaza maji katika vijiji vinavyopitiwa na bomba hilo. Fedha kwa ajili ya mradi huo zilikuwa zimetolewa na kuwa utekelezaji wake umepangwa kuanza mwezi ujao.
Wanakijiji waliposikia jibu hilo walishangilia na kumshukuru Kinana kwa kupita hapo kwani asingepita wasingesikia kuhusu habari hiyo nzuri kwao.
Haya ni baadhi ya mambo ambayo Kinana anayafanya ambao yanakirejeshea CCM nguvu yake ambayo ilipotea kutokana na kukomaa kwa upinzani na kutokana na migogoro ya ndani ya chama. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa CCM kinavizidi vyama vya upinzani katika medani ya siasa, kwani vyama hivyo navyo vimekuwa vikiendelea na mikakati yake ya kuhakikisha kuwa vinaiondoa madarakani kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu 2015.

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf