
Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Magomeni ambayo kwa sasa ni makumbusho ya Taifa
Wakati Taifa linaadhimisha miaka 13 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, pia anakumbukwa kwa namna alivyoona umuhimu wa kununua kiwanja na kujenga nyumba yake mwenyewe, eneo la Magomeni mkoani Dar es Salaam.
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki.
Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake Mustafa Songambele amtafutie
kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho ambacho sasa ipo nyumba
ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.
Mhifadhi Malikale anayesimamia nyumba hiyo,
Emmanuel Katoroki anasema si serikali iliyoamua kuifanya nyumba hii kuwa
makumbusho bali Mwalimu Nyerere mwenyewe, ambaye alitaka Watanzania
wajue ilipotoka historia yake kisiasa.
Katoroki anasimulia kuwa Mwalimu Nyerere baada ya
kupata tetesi kuwa anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alitafuta sehemu
ya usalama na ndipo rafiki yake alipomtafutia kiwanja hicho kilichopo
Magomeni, Mtaa wa Ifunda.
“Mwalimu alikinunua kiwanja hiki mwaka 1957. Hii
ilikuwa ni baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuwa Waziri Mkuu na
wakati ule alihitaji ulinzi kwa kuishi katika mazingira salama, kwa kuwa
Magomeni enzi zile ndiyo ilikuwa kama Masaki sasa hivi, akanunua na
kuanza ujenzi,” anasema Katoroki.
Ulinzi wake
Katoroki anasema kwa wakati ule ulinzi ulikuwa
mdogo hivyo kwa mtu anayeanza kuchipukia kisiasa tena anayetajwa kuweza
kushika nafasi kubwa katika nchi, alihitaji kujilinda kwa kuwa lolote
lingeweza kutokea.
Aidha, Katoroki anasema historia ya kisiasa ya
Mwalimu ilianza wakati akiishi katika nyumba hii na baada ya kuteuliwa
kuwa Waziri Mkuu kwani baada ya hapo alikwenda kuishi katika nyumba ya
serikali Sea View na baadaye Ikulu.
“Pia ni nyumba ya kihistoria kwani aliijenga kwa
kiinua mgongo chake baada ya kuacha ualimu pale Shule ya Sekondari ya
Pugu. Baada ya kuwepo tetesi na pengine mwenyewe alikuwa na taarifa
kamili, aliamua kuachana na ualimu, “ anasema Katoroki.
“Ninasema historia yake kisiasa ilianzia katika
nyumba hii kwani aliamkia katika nyumba hii kwenda kuapishwa kuwa Waziri
Mkuu na kuanza rasmi shughuli za kisiasa na ukombozi wa bara la
Afrika,” anasema.
Kingine ambacho kinaifanya nyumba hii kuwa ya
kihistoria ni pamoja na kuwa alijinyima wakati akijenga, aliishi kwa
muda wa miezi minane tu kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa
Tanganyika Januari 1, 1960.
Katoroki anasema pamoja na nyumba hiyo kuwa ya
pekee, Mwalimu aliwahi kuiuza baada ya kutokea mgogoro katika familia
yake iliyokuwa ikiiogombea.
“Inavyoonekana Mwalimu baada ya kuwa Waziri Mkuu aliitelekeza
nyumba hii na ndugu wakaanza kuigombania. Mwenyewe baada ya kupata
taarifa hizo aliamua kuumaliza ugomvi wa ndugu kwa kuiuza,” anasema
Katoroki.
Hata hivyo historia nyingine iliandikwa mwaka 1973
wakati Jumuiya ya Wafanyakazi (JUWATA), ikitimiza miaka 10 tangu
kuanzishwa kwake ambayo Mwalimu Nyerere alialikwa kuwa mgeni rasmi
katika sherehe hizo na Jumuiya hiyo iliamzawadia nyumba.
“Juwata walimwambia Mwalimu tunataka kukupa
zawadi, alipoifungua alikuta ni hati ya nyumba yake ambayo aliwahi
kumuuzia mtu mwingine,” anasema Katoroki.
Viongozi wa Juwata walimnunulia Mwalimu Nyumba
hiyo kutoka kwa mtu aliyemuuzia kwa Sh 35,000 na kumrudishia mwenyewe
kwa njia ya zawadi.
Aliwashukuru kwa kuirudisha mikononi mwake. Hata
hivyo alisema asingependa ibaki kwenye mikono yake kwani inaweza
kurudisha matatizo aliyoyakwepa na hivyo akaamua kuitoa kwa serikali ili
iifanye kuwa Nyumba ya Makumbusho.
Serikali kwa muda mrefu iliitelekeza nyumba hii na
hivyo kuanza kuharibika na vyombo kuanza kupotea. Hata hivyo, Wizara ya
Utamaduni ilipewa jukumu la kuisimamia nyumba hii chini ya Idara ya
Mambo ya Kale na mwaka 2002 ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na
Utalii chini ya Idara ya Mambo ya Kale.
Vitu vyake
Pamoja na kuwa vitu vingi vya Mwalimu vilipotea
baada ya Mwalimu Nyerere na familia yake, ndani ya nyumba hiyo vipo
vitanda vya familia kikiwamo kile alichokilalia mwalimu mwenyewe kabla
ya kuhama.
Vitu vingine vilivyopo ni kabati la jikoni, kabati
la kuhifadhia fedha (kibubu), pasi ya mkaa, mtungi wa kuhifadhia maji,
redio ya mbao, makochi, cherehani na vyombo vya jikoni.
Pamoja na vyombo ndani ya nyumba hiyo, kuna noti
za pesa zilizokuwa zikitumika enzi za utawala wake. Pia vipo vitabu
alivyowahi kuandika kama vile; Ujamaa ni Imani, Maendeleo ni Kazi,
‘Education to Self Relience’, Tujisahihishe, Tanu na Raia, ‘Our
Leadership and Destiny of Tanzania’ na vingine vingi.
Vitu vingi vilivyopo ndani ya nyumba hiyo
vilipatikana kutoka kwa Mzee Omary (Aliyekuwa baba mlezi wa Mwalimu
Nyerere), ambaye inadaiwa kuwa baada ya kuona nyumba haina mwelekeo
alivichukua na kwenda navyo Dodoma ambako anaishi mpaka sasa.
“Mzee huyu ametunza vitu vingi vya Mwalimu na kama
unavyoona humu ndani, hivi vyote tumevipata kwake, tunasikia kuna
vingine walichukua ndugu na sasa wameviuza kwa watu wa makumbusho
binafsi,” anasema Katoroki.
Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata,” anasema Katoroki.
Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata,” anasema Katoroki.
No comments:
Post a Comment