
Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaja hadharani mishahara ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, serikali imekataa kuizungumzia mishahara hiyo.
Msimamo wa Serikali kutotaja mishahara ya viongozi
wakuu unatofautiana na utamaduni wa nchi nyingine kama Marekani, Afrika
Kusini, Ufaransa na Kenya ambazo mishahara ya wakuu wake huwekwa wazi
kwa umma.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
akiwa wilayani Igunga Mkoani Tabora, alisema Rais Kikwete anapokea zaidi
ya Sh30 milioni kwa mwezi (sawa na Sh360 milioni kwa mwaka) ikiwa ni
marupuru na mshahara kwa mwezi bila kodi, huku Pinda akipokea Sh 26
milioni kwa mwezi.
Akizungumza kwa simu jana, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani
alisema kiongozi yeyote haruhusiwi kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa
kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya utumishi wa umma.
“Kuutaja mshahara wa mtu mwingine ni kinyume cha
sheria na kosa, siyo utaratibu. Kwani wewe upo tayari watu waujue
mshahara wako?” alihoji.
Aliongeza kuwa ingawa mishahara ya viongozi hao
inatokana na kodi za wananchi, sheria ndiyo inayozuia watu kuyataja
malipo hayo hadharani na kwamba hayupo tayari kuutaja mshahara wa rais
au kiongozi mwingine labda mtu huyo autaje yeye mwenyewe.
“Siwezi kutaja mshahara wa bosi wangu wala wa kwangu mwenyewe. Wewe unaujua mshahara wa Obama (Rais wa Marekani)?” alihoji tena.
Akizungumzia mishahara ya marais wa nchi nyingine
duniani kuwekwa wazi, Kombani alisema kila nchi ina utaratibu wake na
kwamba Tanzania haijafikia hatua hiyo.
Alipotafutwa kulizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue simu yake ya mkononi iliita bila
kupokewa.Nae Naibu Mtendaji Mkuu mwenye
jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo Ofisi ya Rais
Ikulu, Peniel Lyimo ambaye alisema yeye si mhusika. “Masuala yote
yanayohusu utumishi yapo Wizara ya Utumishi,” alisema Lyimo.
Akianika mshahara wa Waziri Mkuu, Zitto alisema
kwamba kiongozi huyo analipwa Sh11.2 milioni kama mbunge, Sh8 milioni
kama waziri na Sh7 milioni kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu, hivyo,
kumfanya kupokea zaidi ya Sh300 milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, Kombani alilionya gazeti hili kuandika taarifa za mishahara ya watu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Bashiru Ally alisema Mwalimu Nyerere aliwahi kutaja mshahara wake
hadharani na kuhoji viongozi wanaotaka mishahara yao isitajwe wanaficha
nini.
Hata wakificha mishahara yao bado wananchi wataona maisha wanayoishi kuwa si safi,” alisema.
Hata wakificha mishahara yao bado wananchi wataona maisha wanayoishi kuwa si safi,” alisema.
Wanaharakati pia wahoji
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
Deus Kibamba alisema siyo kosa kwa mtu yeyote kutangaza mshahara wa
viongozi wa umma kwa kuwa wanalipwa kutokana na kodi za wananchi.
Aliongeza kuwa kuanzisa sasa atakuwa balozi wa
kutangaza mishahara ya viongozi hao, ili kila mwananchi aweze kufahamu
kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika nchi nyingine duniani.
“Ninachojua mimi ni kuwa dhana ya mshahara inataka
kuwepo na siri baina ya mwajiri na mwajiriwa, lakini si kwa viongozi wa
umma ambao wanalipwa na kodi za wananchi. Kuanzia sasa hivi nitakuwa
balozi wa kutangaza mishahara ya viongozi hao ili kila mtu ajue,”
alisema Kibamba.
Katibu Mkuu wa Tanzania Labor Party (TLP),
Jeremiah Shelukindo alisema ni vyema kila mtu akaheshimu sheria
inayozuia kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa kuwa kitendo hicho
kinaweza kuwaudhi baadhi ya viongozi wa umma.
“Si vizuri kuingiza siasa kwenye mambo ya
mishahara. Siyo mara ya kwanza kusikia watu wakijaribu kutaja mishahara
ya watu wengine huko ni kukiuka sheria,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa asasi ya Sikika, Irenei Kiria
alisema umefika wakati ambapo inabidi uanze kufanyika mchakato wa
kuzibadili sheria zinazolenga kulinda masilahi ya viongozi wa umma.
“Tunataka kujua viongozi wanalipwa shilingi ngapi na kwa nini wanalipwa kiasi hicho,” alisema Kiria.
Nchi nyingine
Nchini Marekani, mshahara wa rais unajulikana tangu mwaka 1789 kiongozi wa nchi hiyo alipokuwa analipwa Dola 25,000 kwa mwaka.
Kuanzia 2001 hadi sasa, Rais wa Marekani analipwa Dola 400,000 (Sh 640 milioni) kwa mwaka, sawa na Sh 53.3 milioni kwa mwezi.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma analipwa Randi 2
,917 038 sawa na zaidi ya Sh400 milioni za Kitanzania kwa mwaka, Rais
wa Ufaransa, Francois Hollande Sh475 milioni, Waziri Mkuu wa Uingereza,
David Cameron Sh338 milioni, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Sh277 milioni
na Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba Sh226 milioni kwa mwaka.
Wengine na malipo wanayopata kwa mwaka ni Marais
wa Urusi, Vladimir Putin, Sh174 milioni, Ellen Johnson Sirleaf wa
Liberia Sh137 milioni, Michael Satta wa Zambia, Sh126 milioni, Rais wa
Angola, Jose dos Santos Sh91 milioni, Rais wa Lesotho, Profesa Pakalitha
Mosisili Sh88 milioni, Armando Guebuza wa Msumbiji, Sh84 milioni na
Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping Sh60 milioni.
Wengine ni Rais wa India, Pranab Mukherjee Sh49
milioni, Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe Sh27 milioni, Naibu Rais wa
Afrika Kusini, Kgalema Mothlanthe Sh331 milioni, Waziri Mkuu wa Namibia,
Nahas Angula Sh160 milioni, huku Baba Mtakatifu wa Kanisa la Romani
Catholic, Papa Benedict XVI akifanya kazi bila kulipwa mshahara.
No comments:
Post a Comment