
SUPASTAA Mreno, Cristiano Ronaldo, ni mwanasoka anayelipwa fedha nyingi duniani kwa sasa. Staa huyo anapokea Pauni 15 milioni kwa mwaka baada ya makato ya kodi na kabla ya malipo ya bonasi nyingine.
Mashahara wake kwa wiki ni Pauni 288,000 akimwacha
kwa mbali mwanasoka aliyesajiliwa kwa uhamisho ghali zaidi duniani kwa
sasa, Gareth Bale ambaye analipwa Pauni 8.3 milioni kwa mwaka.
Lakini, mara nyingi imekuwa ikisikika juu ya
wachezaji wa nafasi nyingine wakiongoza kwa kusajiliwa kwa fedha nyingi
na kulipwa mishahara mikubwa, lakini si makipa. Ushawahi kufikiria ni
kipa gani analipwa fedha nyingi kwa sasa?
Makala hii inazungumzia makipa wanaolipwa fedha
nyingi kwa mwaka katika klabu zao na kuweka rekodi. Achana na makipa
kama Joe Hart, David De Gea, Pepe Reina, Hugo Iloris na Salvatore
Sirigu, kuna makipa watano bora wanaovuta mshiko wa nguvu.
5. Victor Valdes - Barcelona
Kipa huyo Mhispaniola ambaye hivi karibuni alisema
ataihama Barcelona mwishoni mwa msimu pale mkataba wake utakapofika
tamati, ni miongoni mwa makipa wanaolipwa pesa nyingi katika klabu zao.
Valdes yumo kwenye tano bora. Kwa mwaka anavuta Pauni 5 milioni kutokana na mkataba wake wa sasa anaoutumikia Nou Camp.
4. Petr Cech - Chelsea
Ni mmoja wa makipa mahiri kabisa katika Ligi Kuu
England kwa muongo uliopita. Kwenye klabu ya Chelsea, kipa huyo wa
kimataifa wa Jamhuri ya Czech analipwa Pauni 5.2 milioni kwa mwaka.
3. Gianluigi Buffon - Juventus
Ni kipa aliyedumu kwenye kiwango bora kwa muda
mrefu. Kwenye klabu ya Juventus, Buffon, anatazamwa kama nembo ya timu
hiyo. Umahiri wake unamfanya kuwa kipa anayeingia mikataba minono
inamfanya awemo kwenye orodha ya makipa wanaolipwa pesa nyingi zaidi
kwenye mchezo wa soka kwa sasa.
Buffon, ambaye kwa sasa amebakiza mwaka mmoja
katika mkataba wake ndani ya Juventus ambayo ni bingwa wa Italia,
analipwa Pauni 5.5 milioni kwa mwaka.
2. Manuel Neuer - Bayern Munich
Ni miongoni mwa watu muhimu wanaoifanya Bayern
Munich kuwa imara kwa sasa na kuendelea kutesa Ulaya ikiwa pamoja na
msimu uliopita kunyakua mataji matatu; Bundesliga, Kombe la Ujerumani na
Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kipa huyo wa kimataifa wa Ujerumani kwa sasa
anashika nafasi ya pili kwa kulipwa pesa nyingi baada ya kuvuta Pauni
5.6 milioni kwa mwaka katika huduma yake anayotoa Allianz Arena.
Lakini, Neuer alitarajia kuongeza mkataba mpya hivi karibuni ambao utamfanya kuwa na thamani kubwa zaidi.
1. Iker Casillas - Real Madrid
Mambo yake si shwari kwa sasa ndani ya Santiago
Bernabeu kutokana na kusugua benchi. Kocha, Carlo Ancelotti, bado
anamsubirisha kwenye benchi staa huyo wa Hispania, lakini jambo hilo
halimfanyi kushindwa kuingiza pesa nyingi baada ya mabosi wa timu hiyo
kumpatia mkataba mnono.
Mkataba wake ndani ya Real Madrid unamshuhudia
Casillas akivuna Pauni 6.3 milioni kwa mwaka na kuwa kipa anayelipwa
pesa nyingi zaidi duniani.
No comments:
Post a Comment