WAKATI Mabaraza ya Katiba yakiendelea na mjadala kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba mpya sehemu mbalimbali nchini, imegundulika kuwapo kwa mikakati ya chini chini ya kujiandaa kugombea nafasi za juu za uongozi wa Tanganyika ndani ya vyama vya siasa; RAI linataarifa. Mikakati hiyo inaendeshwa huku kukiwa na kampeni zinazofanywa na vyama hivyo kuhakikisha vipengele vinavyowapa nafasi ya kufanya hivyo vinapitishwa na Mabaraza ya Katiba ili viwemo kwenye Katiba mpya.
Nafasi mpya inayowavutia wengi ni ya kiongozi (rais) wa Jamhuri ya Tanganyika; nafasi iliyopotea kwenye ulingo wa siasa baada ya muasisi wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere kwa kushirikiana na Sheikh Abeid Amani Karume kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964.
Nyerere ndiye aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika. Mapendekezo ya Rasimu ya Katiba hayajaweka wazi bado kiongozi wa Tanganyika ‘mpya’ na wa Zanzibar iwapo atajulikana kama Rais, Waziri Mkuu au Gavana, lakini hilo halijawazuia wanasiasa kufikiria kuijaza nafasi hiyo inayodaiwa kuwa ‘nyeti’.
Wabunge kadhaa wa Tanzania Bara waliozungumza na RAI kwa nyakati tofauti waliweka wazi kuwa vyovyote atakavyoitwa, mtu atakayeshika wadhifa wa juu zaidi Tanzania Bara (Tanganyika) atakuwa na nguvu (madaraka) zaidi kwa kiasi fulani kuliko Rais wa Shirikisho (Muungano).
Wengine walikwenda mbali hata kuanza kushawishiana wao kwa wao kuangalia namna watakavyoweza kugombea na kupata ubunge ndani ya Bunge la Tanganyika na si la Shirikisho, wakiamini humo watakuwa na nguvu zaidi ya kuendesha nchi.
Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikionekana kuwa bado usingizini na kujiaminisha kuwa kampeni zake za kupinga Serikali tatu zitafanikiwa, mmoja wa wanachama wake waandamizi, Jaji Mark Bomani anapingana na hoja hiyo, akiamini kuwa wakati umewadia wa kubadili mfumo wa sasa wa Serikali mbili uliodumu kwa miaka 49.
Jaji Bomani alishiriki kuandaa katiba ya wali ya Muungano akiwa kama Mwanasheria Mkuu miaka ya 1960, amekuwa karibu na Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi na hata walioandaa Rasimu ya Katiba mpya wapo naye karibu.
Kwa usoefu wake, mwanasheria huyo amewahi kusema kwamba ingawa Bara watu hawausemi sana Muungano, bado wangependa kuiona Tanganyika ikiwa na Serikali yake, na majuzi akiwa Zanzibar alinukuliwa akisema kuhusu Serikali tatu:
“Si gharama kubwa kuendesha Serikali tatu kama wengine wanavyodhani na kuamini.”
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba kwa kuwa aliwahi kugombea urais wa Muungano mwaka 1995 na kushindwa kwenye kura za maoni, huenda safari hii akaamua kugombea urais wa Tanganyika, hivyo kuwa Rais wa Kwanza wa Tanganyika baada ya marekebisho ya Katiba; ikiwezekana hata kwa kupitia ugombea binafsi.
Mwingine anayetajwa kuwa na nafasi ya kugombea Urais wa Tanganyika ni Mchungaji Christopher Mtikila, hasa kwa kuwa ni yeye aliyeasisi madai ya kuwa na Tanganyika huru mwanzoni mwa miaka ya 1990, huku pia akipeleka mahakamani na kushinda kesi ya kutaka kuwapo kwa mgombea binafsi.
Sasa Rasimu ya Katiba inataka kuirejesha Tanganyika; nchi ambayo Mtikila anaamini walipewa Watanganyika peke yao na hakuna mwenye mamlaka ya kuwanyang’anya, hivyo kuaminika kuwa huenda akawa mgombea stahiki wa nafasi hiyo.
“… hilo ni kongwa la utumwa kwa Watanganyika. Tunachofanya kwa sasa ni kuandaa ‘petition’ twende mahakamani kupinga mchakato mzima wa kuijadili Rasimu ya Katiba.
“Tunataka Mahakama itupe Tanganyika yetu kwani hatujawahi kuwa nayo kamili yenye mipaka yake na watu wake. Nini Muungano? Tuna haja ya kuwa nao? Hapana. Tunataka Tanganyika.
“Ndio maana Mandela aliwahi kusema kuwa ‘we do not want golden chains, what we need is freedom’ (hatutaki minyororo ya dhahabu, ila uhuru). Kwa nini tufungwe na minyororo eti tu kwa kuwa inang’ara? Hatutaki. Tunataka kuwa huru,” alisema Mtikila, akimaanisha kuwa kwa hali ilivyo sasa hana mpango wa kugombea urais wa Tanganyika.
Ndani ya chama kikuu cha upinzani, Chadema, mkakati uliopo ni wao kuchukua ‘nchi nzima’ ukiondoa Zanzibar ambako hawajafanikiwa kuweka mizizi.
Kauli zinazotolewa na viongozi wa juu wa chama hicho huku wakiendelea kupigia debe kupitishwa kwa Rasimu ya sasa inayotaka Serikali tatu, zinaonyesha wazi kuwa wapo tayari, wamejizatiti kwa mabadiliko hayo.
“Haijawekwa wazi sana lakini nionavyo mimi ni kwamba Mbowe (Mwenyekiti wa Chademea Taifa, Freeman) atagombea Bara (Tanganyika) wakati mzee mzima Slaa (Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad) atagombea Muungano (Shirikisho).
“Ninakuhakikishia wote hawa watapita kila mmoja alikogombea na nchi itakuwa mikononi mwetu iwapo Rasimu hii itapita,” alisema Mbunge mmoja wa Chadema bila kutaka kutajwa jina gazetini, akidai kwamba huo ni mchanganuo binafsi, haujajadiliwa na chama hata kama unazungumzwazungumzwa kwenye makorido ya ofisi za Chadema.
Mbowe na Dk. Slaa wanafahamika vyema Bara na Visiwani kwani wote wawili kwa nyakati tofauti wamewahi kugombea urais wa Muungano na kutembea nchi nzima kwa helikopta; Mbowe mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Jakaya Kikwete na Profesa Ibrahim Lipumba huku Slaa akigombea mwaka 2010 na kukamata nafasi ya pili nyuma ya Kikwete.
Swali linabaki kuwa, ni nani ataandika historia ya kuwa Rais wa Kwanza wa Tanganyika baada ya Nyerere!
No comments:
Post a Comment