
Baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamemkosoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kutamani kung’olewa kwenye nafasi, wakidai kuwa kauli yake inaonyesha jinsi alivyo mpole na dhaifu kiutendaji .
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ayezungumza na gazeti hili jana kwa njia
ya simu alisema kuwa kauli ya Waziri Mkuu Pinda imeonyesha kwamba ana
tatizo la kutokujiamini.
“Kazi za Waziri Mkuu zinajulikana wazi kwamba ni
majukumu mazito ikiwemo kusimamia utendaji wa Serikali kwa kila wizara,
hivyo kusema asihukumiwe kwa sababu ya wizara chache zisizofanya vizuri,
inaonyesha ameshindwa majukumu yake. Alichotakiwa kufanya kwa wizara
hizo ni kumshauri Rais awaondoe madarakani wasiowajibika,” alisema.
Alisisitiza: “ Hatutegemei kumwona Waziri Mkuu
akiingia kufanya kazi kwenye kila wizara, isipokuwa anatakiwa kumshauri
Rais ili mambo yaende sawa.”
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema kuwa amekuwa akifuatilia kauli
za Waziri Mkuu Pinda hata anapokuwa kwenye ziara za kikazi, ambapo
amekuwa akitoa kauli za kuwabembeleza watendaji, hata wanapoboronga.
“Waziri Pinda ni mpole, amepatikana kutokana na
mfumo mbaya wa upatikanaji wa mawaziri uliopo nchini. Kwa wenzetu,
waziri mkuu huchaguliwa mtu aliye jasiri, anayeweza kuongoza nchi kwa
kusimamia shughuli mbalimbali Rais ananapokuwa nje ya nchi,”alisema na
kuongeza:
“Waziri Mkuu akiwa dhaifu ni tatizo, hatujawahi
kuwa na waziri mkuu mzuri tangu alipokufa Moringe Sokoine mwaka 1984,
yeye alikuwa tofauti. Huu ni wakati mzuri wa kuweka hata kwenye
marekebisho ya Katiba, kiwepo kipengele cha sifa za mawaziri, kwa
sababu, wapo wengine unashangaa hata kigezo kilichotumika kumpa nafasi
hiyo lakini ukifuatilia ni urafiki.”
Naye Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam alisema anaona alichozungumza Waziri Mkuu Pinda ni sawa
kwa kuwa angeweza kutangaza kujiuzulu, lakini ametoa nafasi kwamba kama
Rais atamwondoa au wabunge watapiga kura ya kutokuwa na imani naye
atashukuru.
Juzi, akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni
mjini Dodoma, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa yupo tayari kuachia ngazi
endapo tu Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo,
atamshukuru Rais kwa kumwambia, ahsante.
Pinda aliliambia Bunge kwamba endapo Rais
hatafanya hivyo, bado wabunge wanayo mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa
kwa njia ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika utaratibu wa
Bunge wa Waziri Mkuu kujibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.
Katika swali lake, Mbunge huyo alisema; Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa akiwa jijini Mbeya kuwa wapo
mawaziri mzigo katika Baraza la Mawaziri.
Katika swali lake la nyongeza, Rukia alisema wakati wanachangia
taarifa ya Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, yupo Mbunge wa CCM
alisema kuwa Pinda ni mzigo namba moja.
“Kuna mbunge, tena wa CCM, alinukuu kauli ya
Katibu Mkuu wa CCM na akasema kama ni mawaziri mzigo basi mzigo nambari
moja ni wewe Waziri Mkuu, unawaambiaje Watanzania?” aliuliza Rukia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia
wizara 20, hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa wizara moja ama mbili kwa
kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki
No comments:
Post a Comment