
Winnie Madikizela-Mandela, (77) aliinama kumbusu Graca Machel (68), kabla ya kukaa katika kiti cha tatu kutoka kile alichokalia mwanamke huyo. Graca Machel alimwambia maneno machache ‘dada yake’ Winnie wakati akimbusu.
Wanawake hao wote wakiwa wamevalia majaketi meusi
na vilemba, walikumbatiana kwa sekunde kadhaa huku Winnie akitabasamu na
Graca akitazama mbele.
Wote wawili wanaheshimika nchini Afrika Kusini
kutokana na sababu mbalimbali. Winnie anaheshimika kwa mchango wake
mkubwa wa kupigania ubaguzi wa rangi; Graca kwa moyo wake wa kujitolea
kumtunza kiongozi wao mpaka anafariki dunia.
Hata hivyo Winnie amekuwa akikosolewa kutokana na
sababu mbalimbali ikiwamo ile ya kuruhusu wapinzani wake wauawe kwa
kuchomwa moto wakitumia mafuta ya petroli na matairi ya magari.
Mwaka 1988 alipatikana na hati ya kumuua kijana wa
miaka 14 ambaye ilidaiwa alimtuhumu kuwa kibaraka, hata hivyo hukumu
yake ilipunguzwa kutoka kuwa kifungo cha miaka sita jela na kuwa faini.
Winnie pia anatuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu
katika ndoa yake iliyodumu kwa miaka 38 ingawa 27 kati ya hiyo hakuwa na
mumewe ambaye alikuwa akitumikia kifungo katika gereza la Robben.
Graca Machel alifunga ndoa na Mandela wakati wa
sherehe yake ya kutimiza miaka 80. Pamoja na kuwa Winnie na Mandela
walitengana, katika kipindi cha ugonjwa wake kilichodumu kwa siku 181,
alikuwa akimtembelea mara kwa mara.
Mjane wa Mandela, Graca,ambaye pia ni mjane wa
Rais wa zamani wa Msumbiji, Hayati Samora Machel, alitumia muda wote
kuwa pembeni mwa kitanda cha Mandela mpaka alipokata roho.
Ndugu wa karibu wanasema, daktari aliposema hakuna
kitu kinachoweza kufanyika kuokoa uhai wa Mandela, Winnie alifika
nyumbani hapo na alikuwepo muda wote mpaka kiongozi huyo alipokata roho.
Tangu Mandela afariki, Winnie amekuwa akionekana
sana tofauti na Graca. Jumapili ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku tatu
tangu Mandela afariki, Winnie alikwenda kusali katika kanisa ambalo
lilikuwa likifanya misa kuu ya kitaifa kumuombea Mandela .
Winnie alikaa pembeni ya Rais Jacob Zuma. Hata
hivyo siku yake iliharibia na Mchungaji, Mosa Sono aliyekuwa akiongoza
ibada hiyo baada ya kumtambulisha kwa jina la Graca. Kwa upande wake
Graca alisali katika kanisa dogo lililopo karibu na nyumba ya Mandela.
Graca ni mdogo wangu
Kwa muda mrefu sasa Winnie amekuwa akisisitiza kuwa hakuna
uhasama baina yake na Graca na anamuona kama mdogo wake kwa kuwa kiumri
pia amemzidi.
Winnie aliwahi kunukuliwa akisema: “Namuita mdogo
wangu, na yeye huwa ananiita dada, hata tunapozungumza huwa maongezi
yanamuhusu mume wetu,” anasema Winnie.
Dunia yamuaga Mandela kwa heshima ya kipekee
Dunia imeamua kumpa heshima ya kipekee Nelson
Mandela kwa mkusanyiko wa aina yake wa kumuaga kwenye kitongoji cha
Soweto, ambapo zaidi ya viongozi 100 wa dunia wanahudhuria ibada hiyo.
Tangu viongozi walioko madarakani mpaka
waliostaafu, halijawahi kushuhudiwa kuwa na watu wengi kiasi hiki; zaidi
ya watu 95, 000 wamefurika uwanjani tangu usiku wa manane kuhakikisha
wanapata nafasi.
Kitongoji hicho cha Jonnesburg ndiko alikokuwa
akiishi Mandela kabla ya kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa miaka 27, kwa
hivyo ni mahala pa kihistoria kutoa heshima za mwisho kwa shujaa huyo
wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Kiasi cha viongozi 100 wanahudhuria, wakiwamo wa
mataifa na Serikali, wafalme au warithi wao, achilia mbali watu wengineo
mashuhuri duniani ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Ban Ki-moon.
Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja
wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma, na wajumbe wa Baraza la Wazee la
Kimataifa aliloliunda mwenyewe Nelson Mandela, akiwamo Rais wa zamani wa
Marekani, Jimmy Carter.
Marekani inawakilishwa na Rais Barack Obama na
mkewe pamoja na marais wa zamani, George W. Bush na Bill Clinton na
mkewe, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Hillary Clinton.
Viongozi wengine ni pamoja na Rais Raul Castro wa
Cuba, Hamid Karzai wa Afghanistan, Waziri Mkuu wa Uingereza, David
Cameron, na Mwana wa mfalme Charles, Rais Pranab Mukhrejee wa India,
Rais Dilma Russels wa Brazil na watangulizi wake wanne ikiwa ni pamoja
na Lula da Silva,
Waziri mkuu wa Italia Enrico Letta, Kiongozi wa
Mamlaka ya Utawala wa Ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas na mawaziri
wakuu wa Norway, Sweden na Canada, kwa kuwataja wachache tu.
China inawakilishwa na Makamu wa Rais, Li Yuanchao
huku Japan ikiwakilishwa na mrithi wa kiti cha mfalme, Mwanamfalme
Naruhito. Ujerumani inawakilishwa na Rais Joachim Gauck. Takriban
viongozi wote wa bara la Afrika wanahudhuria pia ibada hiyo.
Ibada kuendelea
Ibada kadhaa nyingine zinafanyika hadi siku ya mazishi ya Mandela katika kijiji walichotokea wazee wake, Qunu, Desemba 15.
Mbali na ibada rasmi ya mazishi, maiti ya Nelson
Mandela imewekwa katika Ikulu kuanzia Jumatano hadi ijumaa
itakaposafirishwa kwa ndege hadi Mashariki ya Cape Town kwa mazishi.
Hatua za ulinzi zimeimarishwa. Afrika Kusini inauzoefu kutokana na maandalizi ya Kombe la Dunia la mwaka 2010.
Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, amesema,”Kila kitu kiko tayari, tumejiandaa tangu miaka mitatu au minne iliyopita.”
Makala hii imeandikwa na Julieth Kulangwa kwa msaada wa vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment