Blogger Widgets

Sunday, 3 November 2013

MAKALA ;Usingizi unavyouzwa kwenye mabaraza Kariakoo


Likitajwa jina Kariakoo, fikra zitakupeleka kwenye eneo lenye watu wengi, harakati lukuki na hata biashara za aina nyingi, misongamano mikubwa ya watu na magari.
Hata hivyo, kama unaipenda Kariako, jipe fursa ya kuitembelea ukianzia saa 12 jioni ambako eneo hilo ambalo ni Soko Kuu lililoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam lina vibweka vingi.
Wakati huo jua linapoanza kuzama, joto la mchana kutwa nalo likapungua, msongamano wa magari unazidi, usafiri unakuwa wa taabu kwa kila mmoja anayenuia kurejea nyumbani mapema.
Ifikapo saa mbili usiku, msongamano unaendelea kupungua, idadi ya watu nayo inapungua na sasa jiji linageuka…watu wengi wanaelekea katika makazi yao mapya na hata ya zamani.
Kwa mfano, safari za kwenda Mbezi, Tabata, Vingunguti, Msasani, Kimara, Mbagala zinaongezeka na kuyaacha maeneo mengi ya katikati ya jiji yakiwa matupu.
Hata hivyo kwa, Kariakoo kuanzia saa tano usiku yapo maisha mapya yanayoanza.
Maisha hayo yana watu wake, mazingira yake, raha zake, upweke wake na shughuli za kila aina ambazo ni wachache wanaozifahamu.
Unapowadia usiku Kariakoo ni jiji jipya kabisa ambalo ratiba zake huwa ni za kimya zaidi, za umakini na pengine hazitabiriki wala hazina uhakika wa kufanikiwa au kutokufanikiwa.
Binafsi, ninafika ndani ya Kariakoo saa mbili na nusu usiku na kukuta shamrashamra zimepungua taratibu mithili ya sauti ya mvua inayoanza kukatika.
Wafanyabiashara waliojipanga katika mitaa ya Msimbazi na makutano ya Msimbazi na Uhuru wanasubiri dakika za lala salama za kupata riziki zao.
Muda huu, vipo vikundi vidogo vidogo vya watu wanaocheza bao, wanabishana kuhusu mambo mengi yakiwamo mpira hasa wa Ulaya au hata siasa huku vicheko vya chini chini vikisikika.
Pembeni yupo muuza kahawa na birika lake la moto linaloendelea kuchemka, huku sinia la kashata likisubiri kusindikiza kahawa hiyo anayouza.
Mamalishe nao tayari wameanza kufunga vifaa vyao tayari kurejea majumbani kwao. Magari machache ya abiria nayo bado yanapita hapa na pale yakimalizia wateja wa mwisho mwisho kwa siku hiyo.
Saa 8:30 usiku, tayari maduka mengi makubwa kwa madogo yamefungwa, nje katika vibaraza vya maduka hayo taa zinawaka na humo ndimo vilipo vitanda vya mamia ya Watanzania.
Ninapojongea katika kibaraza kimoja kilichopo Mtaa wa Swahili ndani ya soko hili la Kariakoo nakutana na macho ya Watanzania hao wakazi wa vibarazani.
Kuna msururu wa vijana saba katika kibaraza hiki ambao wamelala mbalimbali bila kusogeleana.
Unaweza kupata taswira ya kutisha kidogo unapowaona kwa mbali kwani wapo katika sare ya mifuko ya salfeti ya rangi nyeupe, jambo ambalo laweza kukupa picha ya kuogofya kidogo.
Ikiwa tayari imeshafika saa tano sasa, mambo yanazidi kunoga.
Ninamwamsha kijana mmoja aliye katikati ya vijana wenzake karibu saba waliokuwa katika kibaraza hicho.
Anaitika na kusema kuwa anaitwa Mussa Athuman au maarufu kama Mangoronyo.
Mangoronyo anayafikicha macho yake kuondoa usingizi na ninapomwomba tuzungumze anakubali na mimi ninaketi juu ya boksi lake ambalo ninabaini hilo ndilo godoro lake kwa miaka 12 sasa.
“Nimekuja hapa Dar es Salaam tangu mwaka 2002 nikitokea Iringa. Nilijua tu kuwa nakuja kutafuta maisha kama ambavyo nilikuwa nasikia kuwa huku zipo biashara nyingi za kufanya,” anasema Mangoronyo.
Hata hivyo, Mangoronyo tofauti na matarajio yake anasema hakuweza kupata ajira kama alivyokuwa akiota.
Badala yake alikaribishwa na wimbi la vijana wenye roho ngumu, waliomwibia baadhi ya nguo zake na fedha kidogo alizokujanazo kutoka kwao Iringa.
 Ikabidi nami nijifunze kuishi kisela kama nilivyowaona wenzangu. Nilipewa orodha ya ajira ninazoweza kufanya, kama kuuza maji, karanga, sigara na pipi, mifuko ya plastiki, lakini pia sikukosa kuambiwa kuwa naweza kudokoa vitu na kupata hela nyingi,” anasema.
Mangoronyo hakuwa na pa kulala wala pa kula na hivyo maisha yake yakawa Kariakoo. Hadi sasa anaishi katika eneo hilo, anakula na kulala Kariakoo.
Fedha anayopata baada ya kufanya vibarua vya kubeba mizigo au kuuza chupa tupu za maji, humtosheleza kwa kula tu, lakini si kuwa na nyumba ya kuishi.
Inapofika jioni, mamia ya vijana hawa wenye makazi yasiyo rasmi katikati ya jiji, huanza kutafuta maboksi ya kulalia ambayo nayo huuzwa.
Wapo watu ambao huyapata maboksi hayo kutoka kwa wenye maduka na kuyauza kwa bei ya Sh100 hadi 200.
Kauli ya Manispaa Ilala
Afisa Habari wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu alisema suala hili ni pana mno hivyo anahitaji kuzungumza na kujadili kwa kina na kitengo cha ustawi wa jamii.
Makazi ya kibaraza kwa Sh500
Katika kibaraza kilichopo Mtaa wa Pemba na Swahili, yupo Awedi Athuman ambaye ametokea Songea, Ruvuma tangu mwaka 2008.
Anasema alitoroka nyumbani kwao akidhani jijini humu (Dar es Salaam) kuna raha na kazi za kufanya zenye mishahara minono, lakini alipofika alimezwa na jiji kubwa linalopendeza lakini lenye mzigo wa dhiki.
Athuman alijikuta akilipia karibu kila kitu ambacho anafanya katika jiji hili. Alitakiwa kulipia kibaraza anacholalia kwa bei ya Sh500.
Kibaraza anacholala kijana huyu kipo katika duka la Osama na malipo hutakiwa kwenda kwa Mzee Kassim, mlinzi wa duka hilo.
“Nilishinda na njaa, kiu mpaka nikaanza kuombaomba, lakini nikagundua kuwa kuombaomba nikiwa nina viungo vyangu hakuna maana. Nikaanza kujiajiri kwa kuwasaidia watu kubeba mizigo yao na wananipa hela,” anasema.
Fedha kidogo anayoipata kijana huyu huishia katika mlo ambao waweza kuwa ni mmoja au akibahatisha miwili kwa siku.
Anatakiwa kuoga, jambo ambalo nalo linahitaji fedha: “Kuoga ni Sh300, kujisaidia 200, yaani sikuwahi kudhania katika maisha yangu kuwa hivyo vitu vinalipiwa, yaani hata kujisaidia,” anasema Athuman kwa mshangao.
Anasema siku akikosa hela basi huzibana haja zake kwa sababu ya hali halisi ya Kariakoo ambayo hakuna mahali pa kujibanza ili ujisaidie.
Mifuko ya salpheti ni shuka
Ndani ya soko hilo, vile unavyodhani wewe kuwa ni taka basi kwa wakazi wa Kariakoo usiku ni bidhaa. Vijana wengi wanaolala katika vibaraza hivi hutumia mifuko ya salpheti kama mashuka yao.
Ni kama sare. Kwani utaukuta msururu wa watu waliojipanga katika kibaraza wote wakiwa na mifuko hii miguuni hadi kiunoni.
Hata hivyo, wapo pia ambao wamekosa mifuko hiyo na hulala na nguo zao tu huku mbu wakiifaidi miili yao.
Licha ya maisha haya, wengi wanaolala Kariakoo usiku wana vitu wanavyomiliki kama nguo, viatu na mswaki.
Kwa mfano, Shariff Mussa amelala juu ya boksi lake lakini kichwani amelalia mto ambao ni begi la nguo zake.
Ndani ya begi hilo kuna mswaki, mashati mawili, matatu na karatasi ambayo ameandika namba za simu za ndugu zake walioko Mbeya.
“Nimesoma mpaka darasa la pili. Ninachokijua ni kuandika, nasoma kwa tabu sana, lakini nipo hapa natafuta maisha, siku nikifanikiwa nadhani nitakuwa na makazi yangu,” anasema Mussa.

Anaongeza kuwa ametumia vibaraza vya Kariakoo kama vyumba vya kulala kwa miaka mitatu sasa tangu alipotoka Kijiji cha Mlalo, Mbeya mwaka 2011.
Kubakwa, kurubuniwa na wahuni
Shariff mwenye umri wa miaka 19 anasema, alikuja akiwa mdogo na ameshuhudia vijana na watoto wadogo wakirubuniwa kwa ajili ya kupata riziki.
Anasema, watoto wa mitaani ambao wamekuja kutoka vijijini na wanaishi katika maeneo ya Kariakoo baadhi yao hurubuniwa na kulawitiwa na vijana wakubwa katika soko hilo.
“Ni tamaa au kudanganywa. Wanafanyiwa vitendo vya ajabu ajabu hapa na wakati mwingine tunashuhudia. Inasikitisha,” anasema Mussa.
Siri ya mifuko inayobeba chupa tupu za maji
Mangoronyo anaeleza kuwa Kariakoo hakuna urafiki zaidi ya salamu au ugomvi.
Hata hivyo, wakazi wa usiku wa kariakoo hawanyimani mbinu.
Mbinu hizo ni zile zinazobuniwa kila siku kuhusu jinsi ya kuiba au kufanya uhalifu fulani.
Mangoronyo anasema, wengi wanaookota chupa tupu za maji, wakati mwingine huiba ‘side mirror’ za magari au taa na kuzitumbukiza katika mifuko hiyo kisha kuendelea na shughuli kana kwamba hakuna kilichotokea.
“Si rahisi kuhisi kuwa mifuko hiyo ina kitu zaidi ya chupa za maji,” anasema.

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf