Watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino) wamewalalamikia wazazi wao kwa kuwatelekeza katika vituo wanavyolelewa baada ya kupelekwa huko kwa ajili ya usalama wao.
Watoto hao wametoa malalamiko yao
kupitia risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, katika
kilele cha Summer Camp waliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la
Under the Same Sun.
Severine Edward ambaye aliwakilisha
wenzake, alisema kuwa kutoka kipindi chwa mwaka 2010 yalipozuka mauaji
ya albino na kupelekwa katika vituo kwa ajili ya ulinzi, wazazi wao
wamewasahau na wamekuwa wakiishi kama yatima.
“Tumekuwa kama yatima tunakumbukwa zaidi na watu baki kuliko wazazi wetu waliotuleta dunia kweli tunaumia sana na matendo yao” alisema Edward.
Katika risala hiyo, aliiomba Serikali
kujitokeza na kuwasaidia misaada mbalimbali kama kuwapatia madaktari kwa
sababu hilo limekuwa ni changamoto kutokana na hali ya ngozi zao.
Alisema kuwa wanaishukuru shirika la
Under the Same Sun kwa kuwa walezi wao wakubwa katika huduma zote
ikiwamo elimu ambapo wamewaweka katika shule ambazo ni salama kwao.
Hata hivyo, mgeni rasmi alisema kitendo
kinachofanywa na wazazi pamoja na walezi kuwatelekeza watoto wao kwa
sababu kuna wafadhili siyo cha kibinadamu na kuwataka kuwa karibu na
watoto ili waweze kupata malezi bora.
Watoto na watu wenye ulemavu wa ngozi
katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikumbwa na adha kubwa ya
kuuawa na kisha kukatwa baadhi ya viungo vya miili yao na baadhi ya watu
wenye imani potofu kuwa viungo hivyo vinawawezesha kupata, mafanikio
hususan katika biashara zao.
Mkoa wa Mwanza ni moja ya mikoa
iliyokumbwa na mauaji ya albino ambao katika kipindi cha mwaka huu jumla
ya albino wanne walivamiwa na kukatwa viungo sehemu mbalimbali za mwili
wao, huku mmoja kati ya hao kufariki dunia.

No comments:
Post a Comment